Home » »

Mwenyekiti CCM atamba kumng’oa Mchungaji Msigwa


MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu (39) amesema anayo nia na uwezo wa kumuangusha katika Uchaguzi Mkuu wa baadaye mwaka huu, Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini anayemaliza muda wake Mchungaji Peter Msigwa (Chadema).
 
Msambatavangu aliyasema hayo jana ikiwa ni wiki moja tangu Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Phillip Mangula afike mjini Iringa kumaliza mgogoro wa kisiasa uliosababisha baadhi ya wanachama wa chama hicho jimbo la Iringa Mjini wafukuzwe uanachama huku Mwenyekiti huyo wa Mkoa akipewa onyo kali.
 
Machi mwaka huu, vikao vya chama hicho ngazi ya wilaya na mkoa viliwafukuza uanachama Shukuru Luhambati, Clara Shirima na Hosea Kaberege huku Msambatavangu akipewa onyo kali lililodaiwa kumuondolea sifa ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi kupitia chama hicho na kuzusha hofu kubwa ya mpasuko ndani yake.
 
Akizungumzia rufaa walizokata na maamuzi aliyokuja nayo Mangula na kuyawasilisha katika kikao cha Halmashauri ya Wilaya ya CCM Manispaa ya Iringa, Msambatavangu alisema; “CCM kwa kutumia kanuni na Katiba yake imepitia rufaa zetu, ikajifunza kitu na kutumia busara yake kutupilia mbali adhabu hizo ili kulinda maslahi mapana ya chama hiki.
 
“Tunajiandaa kushiriki Uchaguzi Mkuu ujao tukiwa wamoja na niwahakikishieni mimi ni mmoja kati ya wana CCM wenye nia ya kugombea ubunge katika jimbo la Iringa Mjini.
 
 “Sijajua makada gani wengine watajitokeza; wenye uwezo wa kusema ni nani ni CCM wenyewe na wananchi wa jimbo hili.
 
"Kwa mimi kutangaza nia na kujitoa nina hakika na ninafahamu nina uwezo wa kupeperusha bendera na kurudi na ushindi, sitakiletea aibu Chama Cha Mapinduzi pamoja na kwamba nipo tayari kumuunga mkono mgombea atakayeteuliwa,” alisema.
 
Alitaja kipaumbele chake cha kwanza endapo CCM itampa ridhaa ya kuwania nafasi hiyo kuwa ni elimu na katika sekta hiyo atahakikisha miundombinu yake inaboreshwa ili iwe ya kisasa.
 
“Nitahakikisha kunakuwepo na ustawi wa elimu, shule bora zenye nidhamu ili Iringa iingie kwenye ushindani wa juu kitaifa.
 
"Tutajiimarisha kujenga mabweni katika shule zetu ili watoto hasa wa kike wawe jirani na shule,” alisema.
 
 Alisema katika kuboresha ustawi wa sekta hiyo atahakikisha vijana wengi wa shule za msingi na sekondari za mjini Iringa wananufaika kwa uwepo wa vyuo vikuu vinne vya mjini hapa kwa kutengeneza ushirikiano utakaosaidia vijana wengi kujiunga na elimu ya juu.
Facebook Blogger Plugin: Bloggerized by Joseph Kipangula Enhanced by Joseph Kipangula

0 comments:

Post a Comment

NURU FM 93.5 IRINGA

.

.

.

Nyali

Pages

Pages

Powered by Blogger.

Blog Archive

Search This Blog