Home » »

Askofu Kanisa Katoliki Amuunga mkono Lowassa .....Asema azma yake ya kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana ndiyo iliyomkuna


ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Rulenge –Ngara, Severine Niwemugizi, amesema anaunga mkono azma ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ya kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana.
 
Sambamba na hilo, amewataka Watanzania kumwomba Mwenyezi Mungu ili awawezeshe kuchagua kiongozi bora na kuonya kauli yake isichukuliwe kuwa ni kumpigia kampeni Lowassa katika safari yake ya matumaini.
 
Akizungumza jana katika jubilee ya miaka 50 ya Seminari ndogo ya Mt. Karoli Lwanga iliyoko Katoke wilayani Biharamulo, Askofu Niwemugizi alisema alianza kumuunga mkono Lowassa katika azma yake ya kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana tangu alipokuwa Waziri Mkuu mwaka 2007.
 
“Tuiombee nchi yetu ipate viongozi makini, waadilifu na wakweli watakaoongoza nchi kwa misingi ya haki na usawa, ambao watajenga jamii yenye kuaminiana na kuheshimiana inayojali mema ya wote, watakaolinda na kudumisha umoja wa taifa.
 
“Najua wewe ndiye muasisi wa shule za kata, sasa zina wanafunzi wengi sana, lakini wanapomaliza kidato cha nne wengi wao wanarudi vijijini na wanajikuta wakikosa ajira. Hii inawatesa sana na wana hasira. Naungana nawe katika kukabili changamoto za vijana ambayo umekuwa ukiizungumzia sana,” alisema Askofu Niwemugizi.
 
Kiongozi huyo wa kanisa pia alimshukuru Lowassa kwa msaada alioutoa wa kutatua mgogoro wa ardhi wa Two Two wilayani Biharamulo wakati akiwa Waziri Mkuu mwaka 2007.
 
Alisema Lowassa alifika Chato mwaka 2007 na kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara na yeye alimwomba asaidie kutatua changamoto ya ardhi.
 
“Ulimwagiza aliyekuwa Waziri wa Ardhi wakati huo, John Magufuli ashughulikie kadhia hiyo na akueleze ardhi hiyo ni ya nani,” alisema Niwemugizi.
 
Akizungumzia mkakati alionao wa kuunga mkono azma ya Lowassa ya kukabiliana na tatizo la ajira, Askofu Niwemugizi alisema atalitumia eneo hilo kujenga chuo kikuu cha kufundisha ufundi stadi na ujasiriamali.
 
“Inaweza kuchukua muda mrefu, lakini hii ni azma yetu. Lengo ni kuhakikisha shule zetu zote jimboni zinatoa elimu ya ufundi pamoja na masomo mengine na watakaofaulu waendelee kupata elimu ya juu ya ufundi stadi ili wajiajiri na kuajiri wengine,” alisema.
 
Awali Askofu Niwemugizi alieleza kuwa jubilee hiyo ilipangwa kufanyika mwaka jana, lakini mgeni rasmi aliyekusudiwa kuwapo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda hakupatikana hivyo waliamua kuifanya mwaka huu.
 
“Ninafurahi na kumshukuru sana Edward Lowassa kukubali mwaliko wangu, tena katika taarifa ya muda mfupi tu akakubali kuja kuwa nasi leo, watu wanaweza kufikiri nimekuita kukupigia kampeni katika safari yako ya matumaini uliyoitangaza kule Arusha Jumamosi Mei 30, watakaotaka kuliona hilo ni juu yao, lakini nafikiri tuna uhuru wa kuchagua,” alisema.
 
Naye Lowassa alipopewa fursa ya kuzungumza, alisema anaomba sala kutoka kwa Watanzania ili Mungu akijalia katika safari yake ya matumaini kazi yake ya kwanza iwe kuunda chombo maalumu kitakachowashirikisha wadau na wataalamu wa elimu.
 
Alisema chombo hicho kitapitia mfumo wa elimu kuanzia elimu ya awali, msingi, sekondari, ufundi na vyuo vikuu ili kupata mwongozo thabiti.
 
“Naamini hamna wasiwasi na usimamizi wangu katika kufanikisha utekelezaji wa mambo ya msingi ya nchi, umefika wakati wa nchi yetu kujibu kwanza swali, tunataka kujenga taifa gani, nini mwelekeo wetu kama taifa kiuchumi, kisiasa na kijamii.
 
“Pamoja na yote uliyosema Baba Askofu, umeeleza matatizo ya elimu kwa ufasaha mkubwa, nami nakubaliana nawe, umefika wakati wa kufanya mabadiliko kwa sababu hata katika mataifa makubwa kama Marekani walipoona elimu yao inaanza kutojibu matakwa ya nchi kwa wahitimu kushindwa kushindana katika soko la ajira, Rais Ronald Regan wakati huo aliunda tume ya elimu iliyokuja na ripoti ya ‘A Nation at Risk’,” alisema Lowassa.
 
Viongozi waliohudhuria jubilee hiyo ni pamoja na Askofu Msaidizi wa Bukoba, Methodius Kilaini, Askofu wa Jimbo la Kayanga, Mhashamu Almachius Rwetongeza, Askofu wa Jimbo la Bukoba na mwangalizi wa Jimbo Katoliki la Singida, Desderius Rwoma.
 
Pia alikuwapo Mkuu wa Wilaya ya Biharamuro, Darry Rwegasira.
Mpekuzi blog
Facebook Blogger Plugin: Bloggerized by Joseph Kipangula Enhanced by Joseph Kipangula

0 comments:

Post a Comment

NURU FM 93.5 IRINGA

.

.

.

Nyali

Pages

Pages

Powered by Blogger.

Blog Archive

Search This Blog