Home »
» KUTOKA BUNGENI: SERIKALI YAPANDISHA PENSHENI KWA 100%
KIWANGO cha pensheni kwa wastaafu walio
kwenye mifuko mbalimbali ya hifadhi ya jamii waliokuwa wakilipwa kima
cha chini Sh 50,115 kinatarajiwa kuongezwa kwa asilimia 100 hadi Sh
100,125.
Naibu Waziri Fedha na Mipango, Dk
Ashatu Kijaji alisema jana bungeni kwamba, wastaafu hao wataanza kulipwa
kiwango hicho kipya pamoja na malimbikizo yao baada ya utaratibu
unaoandaliwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Mifuko hiyo (SSRA) kukamilika.
Kijaji alisema hayo wakati akijibu
swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Conchester Rwamlaza
(Chadema), aliyetaka kufahamu ni lini wastaafu wataanza kulipwa fedha
hizo. Mbunge huyo alisema tangu bajeti inayoisha ya mwaka 2015/16,
serikali kupitia wizara ya fedha iliahidi kupandisha pensheni kwa
wastaafu wanaolipwa Sh 50,000 ili walipwe 100,000.
Alisema ahadi sasa, haijatekelezwa kwa
wastaafu hao, jambo linaloleta usumbufu na wao kushindwa kufahamu ni
lini wataanza kulipwa fedha hizo. Naibu Waziri Fedha na Mipango, Kijaji,
alikiri kwamba wastaafu wote kwenye mifuko wanaolipwa kima cha chini
cha pensheni cha Sh 50,000 kuanzia Julai ,2015 walipaswa kulipwa kima
kipya.
“Ni kweli serikali ilitekeleza ahadi ya
kuongeza kima cha chini cha pensheni kufikia 100,125.85 kutoka Sh
50,114.43, tangu agizo hilo lilipotolewa Julai mwaka jana ni Mfuko wa
Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) pekee ndio ulioanza kutekeleza
agizo hilo kuanzia Julai mwaka jana,” alisema.
0 comments:
Post a Comment