Home » » AFAP YALETA NEEMA KWA WAKULIMA WA MKOA WA IRINGA

AFAP YALETA NEEMA KWA WAKULIMA WA MKOA WA IRINGA


TAASISI ya Africa Fertilizer and Agriculture Partnership (AFAP) imeingia mkoani Iringa ikilenga kuwanusuru wakulima na adha ya ucheleweshaji wa mbolea wanayokutana nayo kila misimu ya kilimo inapowadia.

AFAP yenye makao makuu yake nchini Afrika Kusini imepanga kufanikisha azma yake hiyo kwa kupitia mawakala wa pembejeo wanaofanya shughuli hiyo mkoani hapa.

Akiutambulisha mradi huo hivikaribuni mjini Iringa, Mkurugenzi wa AFAP nchini, Dk Mshindo Msolla alisema pamoja na kuwawezesha mawakala kimitaji, AFAP itawasaidia kujenga maghala ya kuhifadhia mbolea.

Moja ya kampuni zilizonufaika na mpango huo mkoani Iringa ni Alpha Agrochemicals Supply ya mjini Iringa iliyochangiwa na AFAP zaidi ya dola za kimarekani 74,000 kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa ghala lenye thamani ya zaidi ya dola za kimarekani 274,000.

Wakulima zaidi ya 74,200 wanatarajiwa kufikiwa kupitia ghala hilo lenye uwezo wa kuhifadhi tani 6,000 za mbolea kwa wakati mmoja. Zaidi ya tani 12,000 za mbolea zinatarajiwa kuuzwa na kampuni hiyo katika msimu huu wa kilimo wa 2014/2015.

“Ili kufanikisha mpango huu mradi utawasimamia mawakala hao, lengo letu ni kuona wakulima wanapata  mbolea kwa wakati huku wananchi kwa ujumla wao wakihamasishwa umuhimu wa matumizi ya mbolea kwa lengo la kuongeza tija,” alisema.

Alisema AFAP imesaini makubaliano na kampuni sita za mbolea zitakazosambaza mbolea hizo kwa mawakala wanaofanya nao kazi na akazitaja kuwa ni pamoja na
Minjingu Mines and Fertilizers Ltd, Yara (T) Ltd, China Pesticides (T) Ltd, Export Trading Group, Premium Agro Chem Ltd na Tanzania Fertilizer Company (TFC).

Alisema mbali na Iringa, mikoa mingine 10 inayonufaika na mpango huo wa AFAP ni Njombe, Ruvuma, Morogoro, Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Mbeya, Rukwa, Katavi na Kigoma.

Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Iringa, Adam Swai aliishukuru taasisi ya AFAP akisema ni matumaini yake itawasaidia wakulima kutatua kero ya kucheleweshea mbolea.

“Wito wangu niuelekeze kwa mawakala watakaofanya kazi na taasisi hii kuwa waaminifu na kutoa ushirikiano ili mpango huu uweze kufanikiwa na hatimaye mipango ya serikali na wakulima katika kuongeza tija katika kilimo ifanikiwe,” alisema.


Katika msimu wa 2014/2015, mawakala 25 waliothibitishwa kufanya kazi na AFAP watasambaza zaidi ya tani 96,000 za mbolea kwa wakulima wadogo zaidi ya Milioni 2 kupitia mtandao wa mawakala wadogo wa vijijini zaidi ya 1,060.
Facebook Blogger Plugin: Bloggerized by Joseph Kipangula Enhanced by Joseph Kipangula

0 comments:

Post a Comment

NURU FM 93.5 IRINGA

.

.

.

Nyali

Pages

Pages

Powered by Blogger.

Blog Archive

Search This Blog