Home » » Mrema Asema Hajutii Kumnadi Rais Magufuli

Mrema Asema Hajutii Kumnadi Rais Magufuli


MWENYEKITI wa Taifa wa chama cha siasa cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema amesema hakufanya makosa na wala hajutii kumnadi Rais John Magufuli kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu kwa sababu alitambua Watanzania wamelamba dume la maendeleo.
Akizungumza na mtandao huu jana mjini Moshi, Mrema alisema Watanzania wamepata mtu wa kuendeleza kazi aliyokuwa akiifanya kipindi yeye wakati akiwa Naibu Waziri Mkuu katika miaka ya 1990, ya kupambana na wahujumu uchumi, wala rushwa na wafanyakazi wazembe.
Mrema alisema Dk Magufuli ndiye mwenye uwezo pekee wa kuyaleta mabadiliko ya kweli yanayohitajika, japo wengi waliamini hayawezi kupatikana ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ndio maana alichukua jukumu la kumpigia kampeni.
Mrema aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Vunjo mwaka 2010 hadi mwaka 2015, alisema anamfahamu vizuri Dk Magufuli tangu akiwa Waziri wa Ujenzi, kutokana na uchapakazi wake, ambapo walisaidiana kujenga barabara za Vunjo, hali iliyosaidia jimbo hilo kuwa na mtandao mkubwa wa barabara zilizojengwa kwa kiwango cha lami.
“Watu walishangaa sana kwa nini nilimpigia kampeni Dk Magufuli, na kumwacha mgombea wangu…nilijua mtu pekee wa kuyaleta mabadiliko makubwa na kweli ni yeye… Kwanza nampongeza sana na nafurahi sana kwa taifa hili linahitaji kiongozi mchapakazi, mwadilifu kama yeye,” alisema Mrema.
Katika kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka huu, akiwa jimboni Vunjo, Dk Magufuli alikutana na Mrema wakati huo naye akiomba kura za ubunge, na alimshika mkono na kumtambulisha akiwa katika moja ya mikutano yake, na Waziri huyo wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi, alimpigia debe mgombea huyo wa urais wa CCM.
Mrema alifanya hivyo huku chama chake, TLP kikiwa kimemsimamisha MacMillian Lyimo kuwania urais wa Tanzania, hali iliyoibua mijadala wakati huo wa kampeni, huku mwanasiasa huyo machachari nchini akitetea msimamo wake huo wa kumnadi Dk Magufuli badala ya Lyimo.
Mrema alisema Uchaguzi Mkuu umeibua rais mwema, mwadilifu na mwenye uchungu na Watanzania wote. Aliwataka Watanzania kuacha ushabiki wa vyama vyao vya kisiasa na kuangalia mtu anayefanya kazi ya kulikomboa Taifa hili, kama Dk Magufuli kwa kumuunga mkono na kumuombea.
Alisema tangu Taifa lipate Uhuru, kwa sasa Tanzania imeandika historia ya kuwa na viongozi mahiri watatu wa kupambana na umaskini, ambapo aliwataja viongozi hao ni Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Sokoine (sasa hayati) na Dk Magufuli.
Facebook Blogger Plugin: Bloggerized by Joseph Kipangula Enhanced by Joseph Kipangula

0 comments:

Post a Comment

NURU FM 93.5 IRINGA

.

.

.

Nyali

Pages

Pages

Powered by Blogger.

Blog Archive

Search This Blog