Andrew Chenge AGOMA Tena Kuhojiwa na Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma.....Aomba Aruhusiwe kukata Rufaa Mahakama kuu.
MBUNGE wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge ameendelea kupambana ili Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, lisiendelee kusikiliza shauri lake, licha ya pingamizi lake kutupiliwa mbali jana.
Chenge
amewasilisha ombi la kukata rufaa Mahakama Kuu dhidi ya uamuzi wa
baraza hilo, uliotolewa jana na kusomwa na Jaji Hamisi Msumi, ukisema
madai yaliyowasilishwa kwenye pingamizi la mbunge huyo, hayalihusu
baraza hivyo shauri linapaswa kuendelea kusikilizwa kama ilivyopangwa.
“Tumeliangalia
kwa makini pingamizi hili (la Chenge) na kuipitia amri ya Mahakama Kuu
inayozuia suala la akaunti ya Escrow kujadiliwa na tumejiridhisha kuwa,
Baraza hili halihusiani na orodha ya watu waliotajwa kwenye amri hiyo
waliyowekewa pingamizi,” alisema Jaji Msumi.
Alisema
baraza hilo limebaini katika amri hiyo, yako makundi yaliyotajwa
kutojihusisha na suala hilo hadi pale Mahakama Kuu itakapotoa uamuzi
katika kesi ya msingi na katika makundi hayo, Baraza hilo la Maadili
halikutajwa.
Alisema
pia pingamizi kubwa, lililowekwa katika amri hiyo ni kuzuia kupelekwa
bungeni na kujadiliwa kwa taarifa ya ukaguzi maalumu wa miamala ya
Escrow na masuala ya umiliki wa IPTL.
“Hivyo basi, Baraza limeona hoja iliyowasilishwa na kukabidhiwa na mlalamikiwa haina msingi, hivyo imekataliwa,” alisema Jaji Msumi.
Chenge ang’ang’ana
Baada ya uamuzi huo, Chenge aliomba kuwasilisha hoja yake ya kukata rufaa akisema, “sina
nia ya kubishana, ila nataka kuwasilisha nia ya kukata rufaa kwenda
Mahakama Kuu, kupinga uamuzi huu wa Baraza ili suala hili litolewe
uamuzi upya”.
Alisema
anashangazwa na wanasheria wa baraza hilo, ambao hawajatumia muda wao
ipasavyo kwa kwenda masjala ya Mahakama Kuu na kupitia amri hiyo ya
Mahakama Kuu na kujiridhisha, kwa kuwa amri hiyo iko wazi, pana na
imegusa maeneo mengi kuliko inavyofikiriwa.
“Naomba
nitumie haki yangu ya kukata rufaa na kwenda Mahakama Kuu, naomba
nipatiwe mwenendo mzima wa kesi, sasa sijui Baraza hili lina utaratibu
wa kukata rufaa au mimi ndio nitalitambulisha suala hili kwa mara ya
kwanza,” alihoji Chenge.
Kwa
upande wake, Jaji Msumi alisema baraza hilo limemruhusu mbunge huyo
ambaye pia aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akate rufaa dhidi
ya uamuzi wa baraza hilo Mahakama Kuu, jambo litakalosaidia pia kuweka
historia ya kisheria.
“Ni
vyema tuachie Mahakama Kuu ambacho ni chombo cha juu kuliko Baraza
hili, ili itueleze kama ni sahihi sisi kuendelea na shauri hili au la,
kwa sasa sina uhakika kama kanuni zimetengwa kuhusu masuala ya rufaa
kwenye Baraza hili,” alisema.
Alisema
endapo Mahakama Kuu itaamua baraza hilo lisiendelee kusikiliza shauri
hilo, shauri hilo halitasikilizwa, lakini ikiamuru liendelee,
litaendelea kumhoji Chenge na kesi yake ya kukiuka maadili ya uongozi wa
umma.
Juzi
Chenge alisomewa rasmi mashitaka yanayomkabili na Mwanasheria wa
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Hassan Mayunga, ambayo ni
pamoja na kutumia madaraka yake vibaya alipokuwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali na kushauri Serikali iingie mkataba wa miaka 20 na kampuni ya
IPTL.
Aidha,
anadaiwa baada ya kustaafu wadhifa huo wa uanasheria mkuu wa Serikali
Desemba 24, mwaka 2005, mwaka 2006 aliingia mkataba wa kuwa mshauri
mwelekezi wa kampuni wa VIP Engineering and Marketing Limited iliyokuwa
na hisa za asilimia 30 kwenye kampuni ya IPTL.
Lakini,
pia mwanasheria huyo anadaiwa na baraza hilo, kuingia mkataba na
kampuni ya VIP, uliompatia manufaa ya kifedha ya Sh bilioni 1.6 kinyume
na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na fedha hizo ziliingizwa
Februari 5, mwaka jana katika akaunti ya mlalamikiwa namba
00120102523901, iliyopo kwenye Benki ya Mkombozi Tawi la St Joseph
jijini Dar es Salaam.
Baada
ya kusomewa mashitaka hayo juzi, mbunge huyo alikataa kesi hiyo
kusikilizwa na kuwasilisha pingamizi hilo la kutaka suala hilo
kutoendelea kusikilizwa kwa kuwa tayari kuna kesi ya msingi Mahakama Kuu
inayoendelea kusikilizwa.
0 comments:
Post a Comment