ZITTO KABWE KUTANGAZA MAAMUZI MAGUMU YA KUJITOA CHADEMA.
MBUNGE
wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, amesema hatma yake kisiasa ndani ya
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) itajulikana katika kipindi
cha mwezi mmoja kutoka sasa.
Raia
Mwema linafahamu kwamba tangazo hilo la kisiasa linahusu mustakabali
wake wa kisiasa ndani ya Chadema, chama ambacho amekitumikia katika
maisha yake yote ya kisiasa tangu akiwa mtoto wa umri wa miaka 16.
Katika
mahojiano aliyofanya kwa njia ya mtandao na gazeti maarufu la Guardian
la Uingereza wiki iliyopita, Zitto alisema kuna kitu kikubwa atakifanya
mwishoni mwa mwezi Machi huu.
“Sijawahi
kufanya kampeni yoyote kubwa ya kisiasa kupitia mtandao wa twitter
katika maisha yangu ya kisiasa, lakini nataraji kuwa nitafanya hivyo
katika muda wa mwezi mmoja kutoka sasa. Fuatilieni tu twitter na
mtaona,” alisema Zitto pasipo kwenda kwa undani.
Gazeti
hilo la Uingereza limeanzisha utaratibu mpya wa kuhoji watu maarufu kwa
kutumia mtandao wa twitter (twit interview) na Zitto alikuwa mwanasiasa
wa kwanza kuhojiwa baada ya kubainika kuwa ndiye anayeongoza kwa kuwa
na wafuasi wengi kwenye mtandao huo hapa nchini.
Akizungumza
na gazeti hili kuhusu nini hasa anataraji kukifanya mwishoni mwa mwezi
Machi kama alivyozungumza na gazeti hilo, Zitto alisema ni mapema kwa
sasa kuweka kila kitu hadharani lakini wakati ukifika kila kitu kitakuwa
wazi.
“Niseme
kwamba kwenye mahojiano yale nilisema hivyo kweli na nakuhakikishia
kuwa kuna tukio litatokea mwishoni mwa mwezi Machi. Ni tukio gani na
linahusu nini bado mapema kusema.
“Ila
naomba kuahidi Watanzania kuwa watafahamu kila kitu kuhusu tukio hilo
wakati ukifika. Hiyo kampeni ambayo itaendeshwa kupitia mtandao wa
twitter na mingineyo, itakuwa ya kisasa na ya uhakika kuliko yoyote
ambayo imewahi kuendeshwa katika historia ya Tanzania, “ alisema.
Zitto
alikataa kusema lolote kama tangazo hilo litahusiana moja kwa moja na
kuhama kwake kutoka Chadema kwenda ACT au chama chochote kingine cha
siasa hapa nchini zaidi ya kusema; “subirini”.
Kwa
sasa, Zitto ni Mbunge na mwanachama wa Chadema kwa sababu tu ya zuio
ambalo Mahakama Kuu kupitia Jaji John Utamwa liliweka katikati ya mwaka
jana la kufukuzwa kwake ndani ya chama hicho kutokana na kikao cha
Kamati Kuu ya chama hicho.
Zitto
na wenzake, Profesa Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba, walifukuzwa na
Chadema kwa madai ya kupanga mapinduzi ya kumng’oa madarakani Mwenyekiti
wa chama hicho, Freeman Mbowe.
Mwigamba
na Kitila wamehamia katika chama kipya cha siasa cha ACT; Mwigamba
akiwa Katibu Mkuu wa muda na mwenzake mshauri na Zitto mwenyewe amekuwa
akihusishwa na chama hicho.
Akizungumzia
mahojiano hayo ya Zitto na Guardian, Dk. Kitila Mkumbo alisema
aliyasoma mahojiano hayo lakini akasema anayejua nini kitatokea mwishoni
mwa Machi ni Zitto mwenyewe.
“Mimi
kama mshauri wa ACT nasema Zitto kama mwanasiasa makini ana mawazo yake
na mipango yake. Mimi nasisitiza tu kwamba kama ataamua kuja ACT basi
tunamkaribisha kwa mikono yote miwili.
“Tunaamini
kwamba yeye ni muumini wa dhana ya Unyerere (Nyerereism) ambayo ndiyo
msingi mkuu wa sera za ACT. Kama ataamua vinginevyo, sisi pia tutamuunga
mkono kwa sababu tunajua itakuwa kwa nia njema,” alisema.
Katika
mahojiano hayo na Guardian, Zitto aliulizwa kuhusu masuala mbalimbali
yanayohusu siasa na Tanzania, ikiwamo changamoto za kisiasa, hifadhi za
jamii na nguvu ya mitandao ya kijamii katika siasa za hapa nchini.
Zitto
alisema silaha kubwa ya maendeleo ambayo Tanzania inayo kwa sasa ni
wingi wa vijana ambao alisema kama watawekewa mipango mizuri na
kuwezeshwa kutumika kwa kadri ya uwezo wao, Taifa litapiga hatua kubwa.
Alisema
fursa hiyo ina hatari yake nyingine kwamba chini ya asilimia 20 ya
Watanzania hawana ulinzi wowote wa Mifuko ya Hifadhi za Jamii, jambo
alilosema ni hatari kwa mustakabali wa Taifa.
Alisema
pia kwamba kwa sasa Watanzania wengi wana ufahamu wa masuala ya
mitandao ya kijamii, lakini akasema idadi ya wanaoitumia ni ndogo; huku
akibainisha kuwa baadhi ya viongozi wa juu wa serikali hawako hata
kwenye mitandao kama twitter.
Zitto
ana wafuasi zaidi ya 200,000 katika mtandao wa twitter akiwa anaongoza
kwa wafuasi; huku katika nchi nyingine barani Afrika wanaoongoza wakiwa
marais, wanamichezo na wanamuziki maarufu kama Didier Drogba wa Ivory
Coast na Wiz Kid wa Nigeria.
0 comments:
Post a Comment