Mama wa mtoto albino aliyetekwa Geita azungumza alivyojeruhiwa na kuporwa mtoto wake.
MAMA wa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi, Yojana Bahati (1), Ester Thomas aliyelazwa katika hospitali ya Bugando akipatiwa matibabu baada ya kujeruhiwa, ameelezea jinsi alivyovamiwa na watu wasiojulikana.
Akizungumza
na mwandishi wetu, Ester (30) alisema alijeruhiwa juzi nyakati za usiku
na watu wasiojulikana mkoani Geita baada ya kumvamia nyumbani kwao na
kumpora mtoto wake mwenye ulemavu wa ngozi.
Akizungumza
kwa shida hospitalini hapo, Ester alisema alivamiwa akiwa amelala na
mtoto wake huyo ambapo walimkatakata kwa mapanga sehemu mbalimbali za
mwili na kisha kutokomea kusikojulikana.
Naye
Mkuu wa kitengo cha dharura hospitalini hapo, Dk Derick David alisema
mgonjwa huyo alipokewa juzi saa nane mchana akitokea mkoani Geita.
Daktari
alisema mgonjwa huyo ambaye hali yake sio ya kuridhisha, alijeruhiwa
sehemu mbalimbali za mwili kutokana na kukatwa panga kwenye paji la uso
pamoja na kukata sehemu ya mfupa wa pua.
“Tunamshukuru
Mungu mgonjwa huyu anaendelea vizuri baada ya kufanyiwa upasuaji kwani
kwa sasa hali yake ni tofauti na alivyopokewa,” alisema.
Alisema
mama huyo anaendelea na matibabu ya majeraha na pia atapatiwa na huduma
ya kisaikolojia kutokana na maumivu makali aliyonayo ya kuporwa kwa
mtoto wake.
0 comments:
Post a Comment