ZIFAHAMU MBINU ZA ADUI SHETANI (9)--PASTOR ABEL ORGENES
Pastor Abel Orgenes wa huduma ya B'' FAMILY. |
UTANGULIZI:
Kwa kuwa imeandikwa “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa” Hosea 4:6a. na pia imeandikwa “Angalia nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung’oa na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza ili kujenga na kupanda”.Yeremia 1:10 na tena imeandikwa “Nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.” Mathayo 16:18b.”
Na kwa kuwa sisi ni Jeshi la Bwana Duniani, jeshi la Bwana lazima liwe hodari sababu Bwana tuliye naye ni Shujaa wa vita; na kwamba Jeshi la Bwana lapaswa kuvaa silaha zote na kutambua uwezo wa Silaha zake katika Mungu lakini pia linajua mbinu mbalimbali anazotumia adui shetani, Jeshi ambalo ni Imara tayari kupigana vita vizuri vya Kiroho kwa ushindi mkuu, na kwamba Jeshi la Bwana linatambua kuwa lina kila sababu ya kushinda na zaidi ya kushinda. Yaani Sisi ni zaidi ya washindi. Sasa basi katika mfululizo huu tunaanza kuchambua mbinu za adui kadri roho wa Mungu anavyotujalia.
9. KUKUCHOCHEA HASIRA ILI UKASIRIKE NA KUJIKUTA UMETENDA KIPUMBAVU ILI ATIMIZE MALENGO YAKE (Kukukasirisha na kufanya hasira ibaki juu)
Hasira ni nini?
Ni hali ya kuwa na hisia/msisimko mkali wa kutofurahiswa wala kuridhishwa na jambo kiasi cha wakati mwingine na ghadhabu kupelekea kuwa tayari kuadhibu, kukaripia, kutamka maneno makali n.k.
Hasira ni msukumo na hisia isiyopendeza ambayo inalenga mtu au kitu, inaleta hisia na mwonekano usiovutia na inakuza hali yake mbaya kutamani kusababisha madhara.
Ni hali mbaya ya hisia katika ukali ambayo ni ya kawaida kwa manadamu na inasumbua akili yetu karibu kila siku. Mtu ameumbiwa hasira? Hali ya uwezekano wa kukasirika imeumbwa ndani ya mtu na inahitaji kudhibitiwa isiwe juu kupita kiwango kulingana na kiwango cha tukio na sababu ya tukio..
Kila mtu hukasirika ?
Kila mtu hukasirika tangu hata akiwa mtoto mdogo sana… Tofauti kati mtu na mtu kuhusu hasira ? Hii ni muhimu sana katika kufahamiana na mtu unayeoana nae – (eneo hili ni la muhimu katika mahusiano na mawasiliano na mashirikiano)
o Mtu mmoja anaweza kuwa na uwezo wa kuzuia hasira yake na mwingine asiwe na uwezo huo,
o Mwingine mwitikio wa hasira yake hupelekea kutaka kujidhuru na mwingine kudhuru wengine,
o Mwingine hasira yake huinuka haraka na kuisha haraka na mwingine polepole ila inakaa muda mrefu, o Mwingine hasira yake haionekani kwa nje ila inakaa ndani kwa ndani anaweza kuwa kimya kumbe hasira imejaa, wakati mtu mwingine anaweza kuitoa kwa kuonyesha wazi.
o Mwingine hutulizwa na mwingine anaweza asitulizwe kirahisi kwa kusemeshwa bora aachwe tu. mwingine itaisha kwa kuombewa au kuambiwa mambo ayapendayo.
o Kuna tofauti kati ya mtu kukasirika na kupiga ukuta na mwingine kukasirika akapiga mtu,
o Mtu mwingine akikasirika anaondoka kwa hasira na mwondoko wenyewe tu unaonyesha amekasirika mwingine unapokasirika anawaondoa watu kwa hasira, sasa hapo anaweza akakuondoa kwa kukufukuza au taratibu lakini huku amekukazia macho kwa hasira au amefumba macho au ameangalia pembeni na shingo imepinda kama vile kichwa kitachomoka wakati wowote na meno kukutafuna…
o Mwingine unapokasirika anaamua kunyamaza na mwingine anakasirika anawaambia watu wanyamaze…ila anataka kuongea yeye…
o Mwingine anapokasirika anakula sana wakati mwingine unapokasirika anaacha/anazira kula na hasa kama aliyemkasirisha ndie aliyepika hicho chakula, tena asipojizuia anaweza kukimwaga au kusema hata chakula chako kibaya kama alionja yaani utamu wa chakula hutoweka na hamu ya kula huondoka kwa muda wote ambapo hasira iko juu…
o Mwingine anapokasirika anapiga ngumi meza wakati mwingine unapokasirika anapiga ngumi pua ya mtu… Sababu za hasira
o Kutarajia hivi halafu hali ikawa hivi kinyume cha matarajio.. Ulidhani unamjua mtu fulan kumbe hukuwa unamjua..sababu hukutarajia afanye anayofanya…
o Wivu – upo wivu wa kawaida, upo wivu usio wa kawaida, upo wivu mkalii sana na hatari kabisa kiasi cha kusababisha Hasira kwa unayemwonea wivu..
o Mtu anapokosa haki yake aliyoivumilia na kusubiria na hasa inapokuwa ameitafuta kwa muda mrefu
o Unapomkataza mtu jambo halafu anaendelea kukufanyia, umemuonya hasikii anakupandisha hasira
o Unapoingia kwenye mashindano ya maneno na mabishanao ya ana kwa ana halafu ndani yake kukawa na dalili au maneno yeyote ya kukushusha kwa dharau…kwa mfano mtu anabishana na kusema sio hivyo mweshimiwa au unabisha na kusema sio hivyo weweee, sio hivyo we mjinga , au sio hivyo we fisadi…
o Unapotaka kitu kwa shauku iliyopitiliza then ukikutana na kikwazo kidogo unawaka (too desperate)
o Tabia mbaya ya mtu unayeshirikiana naye, tabia inayokera na kukwaza, tabia mbaya ya mtoto, tabia mbaya ya inayokuathiri …na kuathiri wengine husababisha hasira…
o Kukasirishwa na mwingine ambaye unajua huwezi kurudisha hasira kwake na unatafuta mtu mwingine hasa mnyonge wako sasa akukosee kidogo hasira zoote za kazini, za mumeo, za boss wako unazimalizia kwa utakayekutana nae kuanzia kwa konda wa daladala, dereva wa taxi, mtu yeyote njiani n.k.
o Mtu mwingine alisema ‘Anger is about what I don’t want’…Hasira inahusu nisichotaka- kwa sehemu hii inachangia. Ukiomba mkate ukaletewa jiwe kwa vyovyote utakasirika ila Mungu wetu atakupa mkate ulioomba. Hasira ni mwitikio wetu kwa hisia za kutofurahishwa ambayo huinuka mara zote tukutanapo na hali isiyotupendeza/ isiyoturidhisha/ kinyume na matarajio yetu. (Anger is a response to feelings of unhappiness, which in turn arise whenever we meet with unpleasant circumstances.)
Mara tunapozuiwa toka kutimiliza matarajio yetu , au kulazimishwa katika hali/mahali na mazingira tusiyoipenda, au tunawekwa katika mpangilio ambao ndio tunataka kuuepuka akili zetu zinachachamaa maramoja na hisia za kutofurahishwa zinapanda na hisia hizi hugeuka kuwa hasira. Sababu nyingine muhimu ya hasira zetu ni kwamba siku kwa siku tunakabiliana na hali nyingi ambazo hatupendi, kila siku twakabili hali ambazo zinatusumbua, zinatuathiri, zinatuumiza.
Hata mabishano na watu wa rika zetu, au hata kusikia habari mbaya kama vile nyumba yetu imeungua au imechomwa moto, au habari za kuibiwa, au hata kifo katika familia…ni hali ya kawaida kwa mtu wa kawaida kukosa furaha na kukasirika, hatuko katika kujitawala kikamilifu tunahitaji kujifunza na tunamhitaji Mungu na zaidi sana tunahitaji kumnyima shetani nafasi katika eneo hili . .
Je Mungu wetu ana hasira, hasira yake ikoje?
Mungu ana hasira kubwa sana ya kutisha sana….usiombe ukakutana nayo ndio maana watoto wa Mungu wakiudhiwa inaweza kumkasirisha Mungu kiasi kwamba twahitaji kuomba msamaha kwa ajili yao ili hasira yake isije ikawaka moto maana huwa inaweza kufuka moshi….kwa ajili hiyo akaitwa ni ‘MOTO ULAO’
Nahumu 1:2-3 Bwana ni Mungu mwenye wivu,naye hujilipiza kisasi, naye ni Mwingi wa hasira; BWANA hujilipiza kisasi juu ya adui zake, huwawekea adui zake akiba ya hasira.
BWANA si mwepesi wa Hasira, ana uweza Mwingi, wala hatamhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe;BWANA ana njia yake katika kisulisuli natufani, na mawingu ni mavumbi ya miguu yake.
Nahumu 1:6 ni nani awezaye kusimama mbele za ghadhabu yake, naye ni nani awezaye kukaa katika ukali wa hasira yake? Hasira yake kali humwagwa kama moto, nayo majabali hupasuliwa na yeye… Nahumu 1:7 Bwana ni mwema, ni ngome siku ya taabu; naye huwajua hao wamkimbiliao. Mstari wa 8 lakini kwa gharika ifurikayo atapakomesha kabisa mahali pake, na kuwafuatia adui zake hata gizani.
Katika Kutoka 4:14 ;Hasira ya Bwana ikawaka juu ya Musa, akasema, Je! Hayuko Haruni, ndugu yako, Mlawi? Kiashirio cha hasira hapa ni swali, yaani si maelekezo wala maoni, yaani ni kama Musa alipaswa kujua hatakiwi kufanya peke yake na kwamba anatakiwa kushirikiana na mwingine tena ambaye ni mlawi, na ndugu…Mungu anamwagiza jambo jamaa analalamika kuwa ana udhaifu Mungu anajibu kwa hasira..na jibu lake liko katika mtindo wa swali – umeona pia mtu akasirikapo huwa anaweza kutumia swali katika kukufanya ujue anataka nini…mfano: kwa hiyo uliona ni bora uchelewe kuja?, Kwa hiyo ndio umeamua kuniacha peke yangu?, ndio ukaona usipokee simu?, Hivi unanisikiliza au?.
Zaburi 78: 49-58 Akawapelekea ukali wa hasira yake Ghadhabu, na uchungu na taabu, kundi la malaika waletao mabaya. Akiifanyizia njia hasira yake; wala hakuziepusha roho zao na mauti, Bali aliiachia tauni uhai wao; Akampiga kila mzaliwa wa kwanza wa Misri, Malimbuko ya nguvu katika hema za Hamu. Bali aliwaongoza watu wake kama kondoo akawachunga kama kundi jangwani. Hao akawachukua salama wala hawakuogopa, Bali bahari iliwafunikiza adui zao. Akawapeleka hadi mpaka wake mtakatifu, Mlima alioununua kwa mkono wake wa kuume.
55 akawafukuza mataifa mbele yao, akawapimia urithi wa kamba nakuwakalisha kabila za Israeli katika hema zao.
56 Lakini walimjaribu Mungu aliye juu, wakamwasi wala hawakuzishika shuhuda zake.
57 Bali walirudi nyuma wakahaini kama Baba zao; wakaepea kama upinde usiofaa
58 Wakamkasirisha kwa mahali pao pa juu, Wakamtia wivu kwa sanamu zao. Ili tusibakie hewani kwa maandiko ya hasira ya Mungu tusome pia :
Zaburi 85:3 -5 Umeiondoa ghadhabu yako yote, umerudi na kuuacha ukali wa hasira yako Mungu wa wokovu wetu uturudishe. Uikomeshe hasira uliyo nayo juu yetu, je utatufanyia hasira hata milele?Utadumisha ghadhabu kizazi hata kizazi? .
Yesu je, mambo gani humkasirisha? Ugumu wa mioyo ya watu ulimkasirisha Yesu na kumhuzunisha - Marko 3:5 Hapo akawatazama wote kwa hasira, akaona huzuni kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao. Kisha akamwambia huyo mtu, "Nyosha mkono wako!" Naye akaunyosha mkono wake, ukawa mzima tena. .
Pia tunaona sehemu zingine kuwa Yesu - Alikasirikia wanafunzi wake walipowakataza watoto wasije kwake. - Alikasirikia mafarisayo na masudukayo kwa mafundisho yao yasiyo sahihi. - alikasirikia matumizi mabaya ya hekalu - aliukasirikia mti ambao haukuzaa matunda akaulaani - alimkasirikia sauli aliyekuwa anaenda dameski kuwatesa wakristo…
o Muhimu hapa ni kuona ni sababu zipi zinamfanya Yesu akasirike, na kumbuka alikuwa ana uwezo mkubwa sana lakini hakuua mtu, wala kuadhibu watu kwa adhabu kubwa, adhabu kubwa sana aliyotoa kwa watu akiwa amekasirika ni kuwachapa kwa kamba …
o Nina wasiwasi leo mtumishi akikasirika anaamuru mtu afe, au kumtakia mabaya makubwa hadi kizazi cha nne mmh. Tunasoma katika Yohana 2:13-17 (pia Matthayo 21:12-13, Marko 11:15-18, Luka 19:45-46)
13 Sikukuu ya Wayahudi ya Pasaka ilikuwa imekaribia; hivyo Yesu akaenda Yerusalemu.
14 Hekaluni aliwakuta watu wakiuza ng’ombe, kondoo na njiwa, na wavunja fedha walikuwa wamekaa kwenye meza zao.
15 Akatengeneza mjeledi wa kamba, akawafukuza wote nje ya Hekalu pamoja na kondoo na ng’ombe wao, akazimwaga sarafu za wenye kuvunja fedha na kupindua meza zao.
16 Akawaambia wale waliokuwa wanauza njiwa, "Ondoeni vitu hivi hapa. Msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa soko!"
17 wanafunzi wakakumbuka ya kuwa imeandikwa wivu wa nyumba yako utanila. (Yesu alikasirikia watu waliokuwa wanafanya makosa na kukataa kumsikiliza Mungu) Shetani naye je? ana hasira? Kwa sababu hiyo, furahini enyi mbingu na vyote vilivyomo ndani yenu. Lakini, ole wenu nchi na bahari, maana Ibilisi amewajieni akiwa na ghadhabu kuu, kwa sababu anajua kwamba siku zake zilizobakia ni chache." Ufunuo 12:12 Shetani akikasirika huwa hadhibiti hasira yake bali huwa anadhibitiwa, lazima umdhibiti ana hasira sana na wewe, angependa umtumikie la sivyo ufe kabisa ukiwa mwenye dhambi wakati wowote .
Je hasira uliyo nayo ni ya Mungu? Au adui kachomeka yake?
Mara nyingi ukiwa umekasirika ni rahisi kufanya jambo litakalokuumiza wewe mwenyewe au kuumiza mwingine, au wengine ambalo hasira zikiisha unajuta kwa nini ulifanya…Kama kuna jambo muhimu maishani ni namna ya kutawala hisia zako za hasira… Mambo mengi ninayoandika hapa majibu yake yote yako katika neno la Mungu, yako katika maandiko.
Biblia inazungumza nini kuhusu Hasira?
Luka 15:25-32 soma yote – hapa nanukuu mstari wa 28: Huyo kijana mkubwa akawaka hasira hata akakataa kuingia nyumbani. Baba yake akatoka nje na kumsihi aingie. Hasira zingine zinasababishwa na ubinafsi na wivu, na kujitanguliza kuliko kuwatanguliza wengine na kutaka kujifurahisha kuliko kumfurahisha Baba.!
1Wakorintho 13:5 Mwenye upendo hakosi adabu, hatafuti faida yake binafsi, wala hana wepesi wa hasira; haweki kumbukumbu ya mabaya, Kumbe kuna kuwa mwepesi kukasirika au mzito kukasirika ….
Eph 4:26 Kama mkikasirika, msikubali hasira yenu iwafanye mtende dhambi, na wala msikae na hasira kutwa nzima. Sasa Kumbe kuna kukasirika bila kutenda dhambi, ila adui anaweza kuku-time kwenye hasira na kukushawishi utende dhambi; biblia inasema ‘usikubali’. Kwa sababu ya hasira ichochewayo na Shetani na Mtu akaikubali hupelekea mtu akampiga mwingine vibaya , akatukana matusi mazito, akafanya uharibifu mkubwa , hata kuua au kusababisha maafa. Au akatoka na kwenda kulewa na kulala na mwanamke mwingine sababu mkewe amemkasirisha, au akalala na ‘house girl’ na akaendelea kufanya mambo yanayomkasirisha Mungu na kukasirisha wengine, na kuumiza familia yako, kanisa lako na kuharibu jamii na kusababisha matatizo yasiyoisha kirahisi. Usikubali. Na kumbe unaweza kukaa ukiwa umekasirika lakini si kwa muda mrefu anayetaka iwe muda mrefu ni adui shetani anazidi kukuchochoea anakwambia - usikubali kasirika mkasirikie hakuna kumchekea hakuna – na wewe unakubali? Usikubali uchochezi wa Shetani.
Waefeso 4:31 Basi, achaneni na uhasama, chuki, hasira, kelele, matusi! Achaneni na kila uovu! Wakolosai 3:8 Lakini sasa mnapaswa kuachana na mambo haya yote: hasira, tamaa, uovu; kufuru au maneno yasiyofaa yasitoke kamwe vinywani mwenu. Inawezekana kabisa kuachana na TABIA ya hasira…na kwamba …kwani hasira ni rahisi kuambatana na maneno yasiyofaa; sasa imeandikwa maneno yasiyofaa yasitoke vinywani mwenu, neno lisilofaa likishatoka halirudi, yaani inakuwa ndio imetoka…utalifutaje? Sasa mshinde adui kwa kujizuia…na adui atajitahidi kukuletea maneno mabaya yasiyofaa wala huna kazi ya kuyatafura sana utakuta mwili wa kale unainuka matusi uliyokuwa unatumia mwanzo yanakuja, na matusi uliyo wahi kuyasikia yanakuja halafu na lugha mpya kabisa unaianzisha kwa msaada wa adui yako mwenyewe…yaani watu wangejua jinsi adui yao ni shetani na wanashirikiana nae sana kama rafiki wakati ni adui wangemwacha mara moja moja, hebu tusaidiane kuwaambia ‘Shetani ni adui na yuko kazini kukuchafua kwa maneno machafu toka kinywani mwako kwa sababu ya hasira nyepesi na ya muda mrefu.’
1Timotheo 2:8 Basi, popote mnapokutana kufanya ibada nataka wanaume wasali, watu waliojitolea kweli na ambao wanaweza kuinua mikono yao wakisali bila hasira wala ubishi. Katika Ibada kusiwe na Ubishi wala Hasira. Jamani ubishi na hasira hadi Ibadani? Kanisani?
Tito 1:7 Maana kwa vile kiongozi wa kanisa ni mkurugenzi wa kazi ya Mungu, anapaswa kuwa mtu asiye na hatia. Asiwe mwenye majivuno, mwepesi wa hasira, mlevi, mkorofi au mchoyo.
Hapa tunaona Sifa moja wapo ya Kiongozi ni muhimu asiwe mwepesi wa hasira sababu yuko kwenye nafasi kubwa ya maamuzi, na maamuzi yake yana athari kubwa sana kwa wengi anaowaongoza moja kwa moja na hata baadhi ya asiowaongoza. Usifanye maamuzi makubwa wakati umekasirika yanaweza kuwa maamuzi hayo yakawa hayatokani na maono, wito, mapenzi ya Mungu n.k.
Waebrania 11:27 Kwa imani Mose alihama kutoka nchi ya Misri bila kuogopa hasira ya mfalme; na wala hakurudi nyuma, kwani alikuwa kama mtu aliyemwona yule Mungu asiyeonekana. Adui yetu ana hasira lakini hatupaswi kuogopa hasira ya adui…hasira ya adui inatisha ila hata akasirike namna gani hakuna kuogopa, hata atishe vipi hatuogopi…
Yakobo 1:20 Mwenye hasira hawezi kutimiza matakwa ya Mungu yaliyo ya haki. Sasa hapa tunaona jinsi Hasira inavyoweza kuleta hasara, hakuna jambo muhimu kama kumpendeza Mungu na haiwezekani kumpendeza Mungu bila kutimiza matakwa yake, wakati huo huo tukiwa na hasira itatukwamisha kumpendeza Mungu…ndio maana imeandikiwa pia kwamba hasira hukaa kifuani kwa mpumbavu.
Ufunuo 11:18 Watu wa mataifa waliwaka hasira, maana wakati wa ghadhabu yako umefika, wakati wa kuwahukumu wafu. Ndio wakati wa kuwatuza watumishi wako manabii, watu wako na wote wanaolitukuza jina lako, wakubwa kwa wadogo.
Ni wakati wa kuwaangamiza wale wanaoangamiza dunia." Kuna hasira ya mtu mmoja kuna hasira ya watu wengi, kuna hasira ya Taifa zima, kuna hasira ya Mataifa.
Hitimisho:
Mbinu ya adui hapa ni anatafuta kukusababishia hata kwa kitu kidogo tu ujikute mara hasira imepanda na unashangaa hazishuki, wakati mwingine hakuna hata sababu ya kukasirika unajikuta umekasirika…na hasira imejaa kifuani hadi unatetemeka na hutaki kushauriwa, hutaki suluhu…ni muhimu kwenda pembeni hasira ziishe…kila hasira ikipanda jaribu kuwaza ni Mungu hapa au shetani… na mara nyingi utakuta ni shetani…
Mithali 15:1 -4 Jawabu la upole hugeuza hasira; Bali neno liumizalo huchochea ghadhabu. Ulimi wa mwenye hekima hutamka maarifa vizuri; Bali vinywa vya wapumbavu humwaga upumbavu, macho ya Bwana yako kila mahali yakimchunguza mbaya na mwema. Ulimi safi ni mti wa uzima; Bali ukorofi wa ulimi huvunja moyo.
o Hasira ndani inaambatana na udhihirisho katika ghadhabu nje hata usoni.
o Epuka kuchochea ghadhabu ya mtu maana inaweza kusabababisha madhara makubwa ambayo hayatabiriki ni nini itatokea… na shetani kazi yake ni kuleta matokeo yanayohusu kuua, kuchinja na kuharibu ikianzia wewe mwenyewe na yeyote anayekuhusu.
Mithali 22: 24 Usifanye urafiki na mtu mwenye hasira nyingi;wala usiende na mtu mwenye ghadhabu nyingi; Sasa jihadhari na mtu ambaye mara kwa mara umeshuhudia hasira na ghadhabu nyingi alizo nazo… ana nyingi kwa hiyo moja ni ya kwako…yaani atakugawia tu ukiongozana naye…Adui atasababisha upate.
Itaendelea Ijumaa ijayo...
NB: Mungu akubariki kwa kupata nakala ya mafundisho haya, hizi ni baadhi ya mbinu za adui kati ya mbinu zaidi ya 100 ambazo zimeandikwa....NA PIA MAFUNDISHO HAYA YAKO KATIKA CD ya kusikiliza....na karibu sana katika kituo cha mafundisho: Bounty Beach Resort, Mji mwema, Kigamboni, kwa daladala kituo ni REDPOT/mbuyuni. Tunakutana kila jumapili kuanzia saa 9 mchana. Kwa mawasiliano zaidi: Facebook: Abel Orgenes - 0715 94 222 1 Email : abelorgenes@yahoo.com Simu : Rebecca Orgenes - +255 715 928 433 Dar es Salaam, Tanzania.
KUNDI LA SPIRIT OF PRAISE LA AFRIKA YA KUSINI KUREKODI DVD YA NNE MWEZI UJAO
Baadhi ya waimbaji wanaounda kundi hilo ni pamoja na pastor Benjamin Dube, Kgotso Makgalema, mwanamama Zanele Fanele a.k.a Zaza, Tshepiso, Omega, pamoja na Spirit of Praise choir pia kundi hilo kama ilivyokawaida yake itawatambulisha waimbaji wapya wawili wanaojiunga na kundi hilo.
Mpaka sasa kundi hilo kupitia album zake tatu limefanikiwa kuchukua tuzo
kama Crown Award mwaka jana, limewahi kutajwa kwenye kinyang'anyiro cha
kuwania tuzo za SAMA, pamoja na kufanikiwa kuuza matoleo yao kwa
kiwango cha gold na platinum na nyimbo zake zimetazamwa zaidi ya mara
milioni 2 na laki nne katika akaunti yao kwenye mtandao wa YouTube.
Kundi hili ni moja kati ya makundi ambayo yanatajwa kuleta upinzani kwa
kundi la Joyous Celebration katika kutengeneza mambo mazuri katika
kumsifu Mungu.
0 comments:
Post a Comment