Home » »

KESI YA DAUDI MWANGOSI YAANZA KUSIKILIZWA, MWANAHABARI AKAMATWA NA KUBAMBIKIZIWA KESI

[Image]
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa, Frank Leonard ( wa nne kushoto mwenye begi ndogo begani) akiwa nje ya mahakama kuu kanda ya Iringa na wanahabari wengine mara baada ya kesi ya mtuhumiwa wa mauaji ya Daudi Mwangnosi kusikilizwa

KESI ya mauaji ya aliyekuwa Mwandishi wa Habari wa Channel Ten Mkoani Iringa, Daudi Mwangosi imeanza kusikilizwa hii leo baada ya kilichoelezwa na upande wa mashtaka kwamba uchunguzi wake umakamilika.

Kama ilivyo ada, makechero wa Polisi wengi wao wakiwa wamavaa kiraia walikuwepo mahakamani hapa huku wakijaribu kuwazuia wanahabari kutekeleza wajibu wao.

Katika mazingira ya kutatanisha, mwandishi wa habari wa gazeti la Habarileo, Frank Leonard ambaye pia ni Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa alikamatwa na askari wanne waliokuwa wamevaa kiraia kwa kile kilichoelezwa kwamba alikuwa akipiga picha mahakamani wakati kesi ikiendelea.

Baada ya kukamatwa Leonard, alifikishwa kituo cha Polisi cha Kati mjini Iringa na kuachiwa huru baada ya kukosekana ushahidi.


Akizungumza na wanahabari baada ya kuachiwa huru, Leonard alisema "wapo baadhi ya askari kwa makusudi wanataka kubomoa mahusiano baina ya wanahabari na jeshi la Polisi ambayo yanaendelea kujengwa na kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi."


Alisema kitendo cha kubambikiziwa tuhuma ndani ya muhimili wa dola unaojitegemea (mahakama) ni kitendo cha uzalilishaji kinachotaka kuaminisha umma kwamba wanahabari ni watu wasiotaka kufuata taratibu za kimahakama.


Alisema akiwa ndani ya chumba cha mahakama hiyo alikamatwa na askari hao bila idhini ya Jaji wa Mahakama Kuu wakati akizima simu yake ya mkononi iliyokuwa katika mtetemo.



"Nilikuwa nazima simu yangu hao askari hao kwasababu wanazojua wao wenyewe waligeuza suala hilo ili lionekane katika sura wanayoitaka na hatimaye wanifungulie mashtaka," alisema.


Alimshukuru Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Iringa, Ngoi kwa kumtendea haki na baada ya kupata ushahidi kufutilia mbali kesi hiyo.

Akizungumza na wanahabari, Msajili wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Iringa, Dunstan Nduguru aliwashangaa Polisi kwa kuingia shughuli za mahakama.

"Hata kama mwandishi huyo angekuwa anapiga picha, haikuwa kazi yao kumkamata mpaka wapewe agizo na Jaji Mfawidhi aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo," alisema.

Pamoja na askari hao kuwazuia wanahabari kuchukua picha mara baada ya mtuhumiwa huyo kufikishwa mahakamani, Nduguru alisema utaratibu wa mahakama unawaruhusu wanahabari kuchukua picha kabla shughuli kabla shughuli za mahakama hazijaanza na baada ya shughuli hizo kwisha.

"Kuwazuia wanahabari kufanya kazi zao kwa utaratibu huo sio sahihi; siku nyingine mkiona kuna dalili ya kupata bugudha kama hiyo naomba mnijulishe ili niondoe mzozo huo," alisema. 

Mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Iringa, Mary Shangali, Wakili wa upande wa mashtka, Adolph Maganga alisema Adolph Maganda alisema kwa kukusudia mtuhumiwa Pacificius Cleophace Simoni anatuhumiwa kumuua Mwangosi kinyume na kifungu cha sheria ya kanuni ya adhabu namba 196 sura ya 16 kilichofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Alisema katika tukio hilo lililotokea Septemba 2, 2012 katika kijiji cha Nyololo, wilayani Mufindi mkoani Iringa, mshtakiwa alifyatua bunduki yake na kusababisha kifo cha marehemu, papo hapo.

Alisema siku ya tukio marehemu alikuwa Nyororo kwa ajili ya kuripoti na kutoa taarifa kwa umma juu ya mkutano uliokuwa ufanywe na katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Alisema mshtakiwa akiwa mmoja wa wafanyakazi wa Polisi, waliwasihi Chadema wasifanye mkutano huo kabla wafuasi wake hawajaanza kurusha mawe kwa Polisi na baadhi yao kupata majeraha.

Kutokana na mzozo huo, wakili huyo wa serikali alisema polisi walipiga mabomu ya machozi ili kuwatawanya wafuasi hao kabla mshtakiwa huyo hajamfyatulia bomu marehemu.

Wakili huyo aliwasilisha ramani ya eneo la tukio, ripoti ya mtaalamu wa milipuko na ripoti ya daktari aliyechunguza mwili wa marehemu Mwangosi na gazeti la Mwananchi la Septemba 3, 2012 lililochapisha  picha ya tukio hilo katika ukurasa wa mbele kama vielelezo vinavyohusiana na kesi hiyo.

Wakili wa upande wa utetezi Lwezaula Kaijage alitaja mambo wanayokubaliana katika kesi hiyo kuwa ni jina na anuani ya mshtakiwa na kwamba marehemu Mwangosi alikufa kifo ambacho si cha kawaida.

Na kwamba mshtakiwa Simoni alikamatwa na amefikishwa mahakamani akihusishwa na mauaji hayo.

Wakili Kaijage alisema vielelezo vingine vilivyoletwa na upande wa mashtaka hawakubaliani navyo kwakuwa vinahitaji ushahidi kutoka kwa wahusika.

Jaji Shangali aliahirisha kesi hiyo mpaka kikao kingine cha mahakama kuu kitakapoitwa ili ianze kusikilizwa.
Facebook Blogger Plugin: Bloggerized by Joseph Kipangula Enhanced by Joseph Kipangula

0 comments:

Post a Comment

NURU FM 93.5 IRINGA

.

.

.

Nyali

Pages

Pages

Powered by Blogger.

Blog Archive

Search This Blog