CHADEMA YAHITIMISHA KURA ZA MAONI UCHAGUZI MDOGO JIMBO LA KALENGA, MWANASHERIA MWENDA AIBUKA KIDEDEA
Sinkala Mwenda akiwa amenyanyuliwa juu baada ya ushindi wa kura za maoni juzi |
MGOMBEA Sinkala Mwenda ameibuka
kidedea wa kura za maoni za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika
mchakato wa kumpata mgombea atakayepeperusha bendera ya chama hicho katika
uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kalenga.
Kura hizo za maoni zilizofanyika juzi
katika ukumbi wa St Dominic, mjini hapa zilishirikisha wagombea 13.
Jimbo la Kalenga liko wazi baada ya
aliyekuwa mbunge wake, Dk William Mgimwa kufariki dunia Januari 1, mwaka huu.
Mwenda mwanasheia aliyemaliza
shahada yake ya sheria katika chuo cha Ruaha Iringa, aliibuka kidedea baada ya kupata kura 132 dhidi ya kura
122 alizopata mshindani wake wa mkuu Grace Tendega.
Kabla ya kura hizo kuanza kupigwa
wajumbe wengi walisikika wakimpigia chapuo, Tendega wakidai ana historia nzuri
ya kisiasa katika jimbo hilo kwa kuzingatia kwamba katika Uchaguzi Mkuu wa 2010
aligombea ubunge katika hilo kupitia chama cha Jahazi Asilia na kutoa upinzani
mkubwa kwa Dk Mgimwa.
Mwingine aliyekuwa akipewa nafasi ni
Zuberi Mwachula ambaye hata hivyo kutokuwepo kwake katika kura hizo za maoni
kulisababisha wajumbe wamuadhibu kwa kutompa kura hata moja.
Pamoja na kurudisha fomu za kuomba
kuteuliwa na chama hicho, Mwachula aliyekuwa Meneja wa Shirika la Kimataifa la
Concern mkoa wa Iringa alishindwa kuhudhuria katika mchakato huo kwa kile
kilichoelezwa kwamba yuko nje ya nchi kikazi.
Naye kijana machachari ambaye ni
wakala na muuza magazeti maarufu mjini Iringa, Aidan Pungili pamoja na kumudu
jukwaa kutokana na uwezo wake wa kujieleza vizuri aliambulia kura 2.
Uchaguzi huo uliomalizika majira ya saa 4 usiku jana ulisimamiwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema Taifa Chiku Abwao
na Mkurugunzi wa Oparesheni na Mafunzo ya chama hicho Benson Kigaila.
Wagombea wengine ambao
wameonyesha kufanya vema
kiasi baada ya kujiunga na Chadema wakitokea
CCM ni pamoja na Dr Evaristo Mtitu
aliyepata kura 32 na Ancent
Sambala kura 22.
Wengine walioshiriki kura hizo na
kura zao kwenye mabano ni Akbar Sanga (21),
Rehema Makoga (4), Henry Kavina (9), Mussa Mdede (48), Mchungaji Samweli Nyakunga (2) na Mwalimu Vitus Lawa akipata
kura (14).
Katika nasaha zake kwa wagombea na
wajumbe, Kigaila alisema ushindi wa kura za maoni sio kigezo pekee
kinachotumiwa na Chadema kupata mgombea.
“Tunataka hili lieleweke, huu ni
mwanzo wa mchakato. Ni lazima tupate mgombea kwa kuzingatia mazingira ya
Kalenga, awe anakubali ndani ya chama na kwa wapiga kura wajimbo hilo kwasababu
tunataka kushinda,” alisema.
Alisema baada ya kura hizo za maoni
Kamati Kuu ya Chadema Taifa itakutana kesho Ijumaa, Februari 14 na kufanya maamuzi ya
mwisho kwa kuzingatia mambo mengi zikiwemo taarifa za kiintelejensia za ndani
ya chama.
“Tuna heshimu sana kura za maoni,
lakini sio kigezo pekee. Watanzania wana imani sana na Chadema,
kitakachotufanya tushinde ni aina ya mgombea tunayempeleka kwa watu, vinginevyo
tunaweza kufanya kampeni kubwa na tukashindwa,” alisema.
Taarifa za awali kutoka ndani ya chama hicho zimedai kwamba katika kampeni zao watatumia helkopta mbili na magari nane ya chama ili kuyafikia makundi ya wapiga kura kwa kasi zaidi.
0 comments:
Post a Comment