PSPF YAIPIGA JEKI SERIKALI YATOA MSAADA WA MADAWATI 100 KWA SHULE ZA MSINGI
Baadhi
ya madawati yakiwa ndani ya lori kabla ya kukabidhiwa kwa shule za
msingi 3 za Mufindi Kaskazini.(picha zote na Denis Mlowe)
SHULE tatu za msingi za jimbo la Mufindi Kaskazini katika
wilaya ya Mufindi mkoani Iringa zimenufaika kwa msaada wa madawati 100
yaliyotolewa na mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) yenye thamani ya
shilingi milioni 5.
Akikabidhi msaada huo kwa mkuu wa wilaya ya Mufindi Monica
Kalalu juzi katika ofisi za Halmashauri ya wilaya hiyo, Afisa Mfawidhi wa PSPF
mkoa wa Iringa Baraka Jumanne alisema lengo la msaada huo ni sehemu ya mpango
wao katika kusaidia sekta ya elimu nchini na kukuza elimu ya shule za msingi katika
wilaya hiyo.
"PSPF ni shirika la mfuko wa pensheni hivyo faida
lazima iifikie jamii hasa katika suala la elimu ya msingi hivyo tumeamua
kuwapatia madawati haya baada ya maombi ya Mbunge wenu Mahamudu Mgimwa kutuomba kumsaidia katika
suala la madawati hivyo tuna kila sababu ya kuwasaidia watoto wetu ili wawe
katika mazingira mazuri ya kupata elimu, ndiyo maana tumechukua jukumu hili,"
alisema Jumanne
Alisema kuwa tatizo la ukosefu wa madawati ni kubwa, hivyo
kila mtu anapaswa kusaidia ili wanafunzi wapate elimu sahihi na yenye ubora na
kuepukana na kukaa chini kwa wanafunzi wa shule za msingi.
Aidha Jumanne alitoa wito kwa wananchi wa wilaya hiyo
kujiunga mfuko wa pensheni kwa watumishi wa umma wa PSPF kwa huduma bora na
mafao bora yakiwemo mafao ya uzeeni,ulemavu,mirathi,mafao ya rambirambi za
mazishi, malipo ya wategemezi na malipo ya penshini ya kila mwezi.
Alizitaja
shule zilizonufaika na msaada huo kuwa ni shule ya
msingi Mjimwema ilipata madawati (40), Mamba shule ya msingi (40) na
shule ya msingi
Kinyanambo (20) na kuongeza kuwa awamu ya kwanza walitoa madawati 250
kwa shule mbalimbali msingi katika jimbo la Mufindi Kaskani na
kuzinufaisha shule zaidi ya 6.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Mufindi Monica Kalalu
alilishukuru shirika la PSPF kwa msaada huo na kutoa wito kwa wanafunzi na walimu
kuyatunza madawati na kuwataka wadau wengine wajitokeze kuisaidia sekta ya
elimu hususani elimu ya msingi kwa kuwa kwa upande wa sekondari tatizo la
madawati limekwisha.
0 comments:
Post a Comment