Home » »

 
                     KILA MTANZANIA ANADAIWA  600,000 SASA
 
Wakati Serikali ikibanwa na wabunge kwa kushindwa kutekeleza Bajeti ya mwaka 2013/14 kutokana na kutegemea fedha za wahisani, Kamati ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara imesema deni la taifa limeongezeka kwa Sh8.2 trilioni kwa kipindi cha miezi saba tu.

Ilisema jana kuwa hadi Juni, mwaka jana deni hilo lilikuwa Sh21.2 trilioni lakini hadi Januari mwaka huu, deni hilo lilipaa hadi Sh29.4 trilioni na fedha hizo zimekopwa kwa ajili ya kuendeshea warsha, semina, safari, mafunzo na matengenezo ya magari.

Akiwasilisha taarifa ya kambi ya Upinzani, Waziri Kivuli wa Fedha, James Mbatia alisema ukiligawanya deni hilo kwa idadi ya Watanzania milioni 45, kila mwananchi atakuwa anadaiwa Sh600,000.

Kati ya Sh5.8trilioni za bajeti ya Wizara ya Fedha mwaka 2014/15, Sh4.3trilioni zimetengwa kwa ajili ya kulipa Deni la Taifa

Akiwasilisha taarifa ya Kamati, Mwenyekiti wake, Luhaga Mpina alisema Sh24.18trilioni ni deni la Serikali, Sh3.75trilioni ni deni la sekta binafsi na Sh1.15trilioni ni deni la Benki Kuu Tanzania (BoT).

“Ongezeko hili la deni haliendi sambamba na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ujenzi wa miundombinu ya uchumi. Hali hii inajenga hofu kuwa huenda deni hili limekuwa ni uchochoro wa ubadhilifu wa fedha za umma,” alisema Mpina.

Alisema licha ya Serikali mara kadhaa kueleza kuwa deni hilo ni himilivu, kuna viashiria vinavyoonyesha kuelemewa kwa taifa na mzigo mkubwa wa madeni.

“Mfano ni mapato ya ndani yamezidiwa na matumizi ya kawaida hivyo kuifanya Serikali kukopa hata kwa ajili ya warsha, semina, safari, mafunzo na matengenezo ya magari,” alisema Mpina.

“Deni la Taifa sasa limefikia asilimia 47 ya Pato la Taifa na kwa kipimo cha bei ya sasa deni la taifa limefikia asilimia 24, huku deni la nje pekee likiwa ni asilimia 19” alisema Mpina na kuongeza:

“Licha ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kuahidi kwa muda mrefu kufanya ukaguzi maalumu wa deni la taifa, hadi sasa taarifa yake haijawasilishwa. Ni lini taarifa hiyo itawasilishwa bungeni ili kuwawezesha wananchi kufahamu undani wa jambo hili?” alihoji.

Kamati hiyo pia iliilipua Serikali kwa kuuza mashine za elekroniki (EFD), kati ya Sh600,000 hadi 700,000 kwa maelezo kuwa kiwango hicho ni kikubwa kwa mzunguko wa biashara ya mtaji wa Sh14 milioni kwa sababu mtaji wake hauzidi Sh5milioni.

Mpina alisema mashine hizo zinatakiwa kugawiwa bure kwa wafanyabiashara wenye kipato chini ya Sh40milioni na kufafanua kuwa chombo hicho chenye taarifa muhimu za mapato ya Serikali hakitakiwi kuuzwa na kufanyiwa matengenezo na mtu binafsi.
Facebook Blogger Plugin: Bloggerized by Joseph Kipangula Enhanced by Joseph Kipangula

0 comments:

Post a Comment

NURU FM 93.5 IRINGA

.

.

.

Nyali

Pages

Pages

Powered by Blogger.

Blog Archive

Search This Blog