Home » » Watoto Wanne wa Familia Moja Wateketea Kwa Moto Wakiwa Usingizini

Watoto Wanne wa Familia Moja Wateketea Kwa Moto Wakiwa Usingizini

HUZUNI imetanda katika wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, baada ya ajali ya moto wa kibatari kuteketeza watoto wanne wa mama mmoja, waliokuwa wamefungiwa chumbani na dada anayewalea.

Ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia jana katika mtaa wa Nyerere, mji mdogo wa Kibaigwa wilayani Kongwa, wakati mama wa watoto hao aliposafiri kwenda shambani Kiteto mkoani Manyara, kwa ajili ya kuvuna mazao na kuwaacha watoto wake mikononi mwa dada, aliyekuwa akimsaidia kuwalea.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, Lazaro Mambosasa alisema chanzo cha ajali hiyo ni mlipuko wa kibatari kilichokuwa ndani ya chumba walicholala watoto hao, ambacho kilichoma godoro na kuteketeza nyumba yote.

Moto huo ulioanzia katika chumba hicho, umeelezwa kuteketeza nyumba yote ya vyumba sita iliyojengwa kwa tofali za udongo mali ya Nelson Mdachi.

Kamanda Mambosasa aliwataja watoto hao kuwa ni Elizabeth Nelson (11) mwanafunzi wa darasa la saba, Samweli Mdachi (7) anayesoma darasa la kwanza na Nase Mgomba (9) anayesoma darasa la pili katika shule ya msingi Miembeni na Peter Lema (9) mwanafunzi darasa la tatu shule ya msingi St Paulo.

Kutokana na ajali hiyo, Kamanda Mambosasa amewakumbusha wazazi wasiache watoto peke yao nyumbani kwa kuwa ni hatari kwani ajali ikitokea ni vigumu kuokolewa.

Taarifa kutoka kwa watu wa karibu na majirani wa familia hiyo, zimedai kuwa mama wa familia hiyo alikwenda shambani kuvuna mazao katika wilaya ya Kiteto, mkoani Manyara na kuwaacha watoto hao chini ya uangalizi wa msichana aliyefahamika kwa jina moja la Ester.

Kwa mujibu wa madai yao, ilipofika usiku Ester anayetajwa kuwa na jukumu la kulea watoto hao, alitoka na kwenda kusikojulikana huku akiwafungia watoto hao kwa nje.

Mkazi wa Kibaigwa, Denis Luhunga, alipozungumza na mwandishikuhusu ajali hiyo alidai kuwa kibatari kilipolipuka, kilisababisha godoro kushika moto na kuteketea kwa watoto hao. 

“Aliwafungia watoto ndani akaacha kibatari kinawaka, baada ya kulipuka moshi mwingi ulijaa ndani,” alidai Luhunga.

Kuhusu alipo baba wa familia hiyo, mkazi mwingine wa eneo la tukio hilo, Paulo Sauli alisema baba wa watoto hao, aliyemtaja kwa jina la Nelson Mdachi, alishakufa miaka mitatu iliyopita na jukumu la kuwalea aliachiwa mama yao.

Alifafanua kuwa baba huyo ambaye wakati wa uhai wake alifahamika kwa jina maarufu la ‘Moja kwa moja’, alikufa baada ya kuanguka kutoka juu ya mti alipokuwa akirina asali na tangu hapo, jukumu la kulea likabaki kwa mama mzazi wa watoto hao.

“Tukio hilo limetusikitisha sana ni tukio baya maana wameteketea kabisa hajulikani nani ni nani,” alisema Sauli na kuongeza, “Hata Ester hafahamiki alipo, kuna watu wengi lakini tumemuangalia hapa msibani hatumuoni.”

Taarifa nyingine kutoka eneo la tukio, zilidai kuwa Mdachi alizaa na mama huyo watoto wawili na baada ya kufariki, mama huyo alizaa watoto wengine wawili na wanaume wengine.
Facebook Blogger Plugin: Bloggerized by Joseph Kipangula Enhanced by Joseph Kipangula

0 comments:

Post a Comment

NURU FM 93.5 IRINGA

.

.

.

Nyali

Pages

Pages

Powered by Blogger.

Search This Blog