Home » » Viongozi Waliosaliti CCM Tabora Wasimamishwa

Viongozi Waliosaliti CCM Tabora Wasimamishwa


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Tabora Mjini, kimewasimamisha viongozi wanne wa Kata ya Chemchem kwa kukisaliti chama hicho katika mchakato uliopita wa kura za maoni hadi Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25 Mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa chama hicho, Kanuth Ndaghine alisema sababu za kuwasimamisha viongozi hao ni kukisaliti chama na kutosimamia kikamilifu uchaguzi katika ngazi za udiwani wa kata hiyo.

Ndaghine alisema viongozi hao walikuwa hawakisaidii chama kupata ushindi bali waliegemea chama pinzani ambacho kiliweza kuchukua nafasi ya udiwani kupitia Chama cha Wananchi (CUF) katika kata ya Chemchem mkoani Tabora.

Aidha alisema wanachama na wananchi hawana imani na viongozi hao tangu kipindi cha mchakato wa kura za maoni mpaka kufikia uchaguzi mkuu. 
 
Hata hivyo, alieleza kusikitikia kitendo kilichofanywa na viongozi hao cha kukisaliti chama kwa kuwa walikuwa na wagombea wao katika mchakato wa kura za maoni ambao kura hazikutosha.

Aliyeshinda ni Elizabert Shoki aliyepata kura nyingi zilizopigwa na wanachama wa CCM katika kata hiyo. Viongozi hao walishindwa kumuunga mkono aliyekuwa mgombea wa chama hicho na kukipigia kura CUF, kitu ambacho hakikubaliki katika chama kwa kuwa wao ni viongozi wa kata hiyo.

Pamoja na CCM kukosa kata hiyo, alisema katibu huyo kuwa viongozi hao hawafai katika chama kwa sababu wanaonekana dhahiri kukisaliti chama hicho na kuwatia aibu wanachama na wananchi kwa ujumla.

Aliwataja viongozi waliosimamishwa uongozi kuwa ni Mwenyekiti wa Kata Juma Mapunda, Katibu Kata Mwajuma Boko, Katibu wa siasa na Uenezi kata hiyo Issa Water na Katibu uchumi na fedha, John Muhando.

Kwa upande wake Katibu wa Siasa na Itikadi, Uenezi Wilaya ya Tabora Mjini, Rashidi Tollu alisema waliwateua viongozi wengine ili kukaimu nafasi hizo za viongozi waliosimamishwa na kuweka wengine.

Waliowekwa ni Kisuzi Mswanyama Mwenyekiti, Tatu Balola Katibu kata, Hussenu Sengo katibu wa Siasa na Uenezi wa kata Selemani Mzee Kaimu katibu wa Uchumi na fedha. Tollu amewataka viongozi hao waliokaimishwa nafasi hizo wafanye kazi kwa uadilifu mkubwa kwa wanachama na wananchi wote kwa ujumla, kwani wananchi wana imani na chama hicho ambacho kinasimamia misingi Imara ya amani,umoja na upendo.

Akizungumzia kusimamishwa kwao, Juma Mapunda alisema hawawezi kuzungumza chochote juu ya kusimamishwa kwao isipokuwa wanaandika barua ili waipeleke kwa Mwenyekiti wa chama hicho, Abdulrahman Nkonkota.
Facebook Blogger Plugin: Bloggerized by Joseph Kipangula Enhanced by Joseph Kipangula

0 comments:

Post a Comment

NURU FM 93.5 IRINGA

.

.

.

Nyali

Pages

Pages

Powered by Blogger.

Blog Archive

Search This Blog