TAASISI
ya Africa Fertilizer and Agriculture Partnership (AFAP) imeingia mkoani Iringa
ikilenga kuwanusuru wakulima na adha ya ucheleweshaji wa mbolea wanayokutana
nayo kila misimu ya kilimo inapowadia.
AFAP
yenye makao makuu yake nchini Afrika Kusini imepanga kufanikisha azma yake hiyo
kwa kupitia mawakala wa pembejeo wanaofanya shughuli hiyo mkoani hapa.
Akiutambulisha
mradi huo hivikaribuni mjini Iringa, Mkurugenzi wa AFAP nchini, Dk Mshindo
Msolla alisema pamoja na kuwawezesha mawakala kimitaji, AFAP itawasaidia kujenga
maghala ya kuhifadhia mbolea.
Moja
ya kampuni zilizonufaika na mpango huo mkoani Iringa ni Alpha Agrochemicals
Supply ya mjini Iringa iliyochangiwa na AFAP zaidi ya dola za kimarekani 74,000
kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa ghala lenye thamani ya zaidi ya dola za
kimarekani 274,000.
Wakulima
zaidi ya 74,200 wanatarajiwa kufikiwa kupitia ghala hilo lenye uwezo wa
kuhifadhi tani 6,000 za mbolea kwa wakati mmoja. Zaidi ya tani 12,000 za mbolea
zinatarajiwa kuuzwa na kampuni hiyo katika msimu huu wa kilimo wa 2014/2015.
“Ili
kufanikisha mpango huu mradi utawasimamia mawakala hao, lengo letu ni kuona wakulima
wanapata mbolea kwa wakati huku wananchi
kwa ujumla wao wakihamasishwa umuhimu wa matumizi ya mbolea kwa lengo la
kuongeza tija,” alisema.
Alisema
AFAP imesaini makubaliano na kampuni sita za mbolea zitakazosambaza mbolea hizo
kwa mawakala wanaofanya nao kazi na akazitaja kuwa ni pamoja na
Minjingu
Mines and Fertilizers Ltd, Yara (T) Ltd, China Pesticides (T) Ltd, Export
Trading Group, Premium Agro Chem Ltd na Tanzania Fertilizer Company (TFC).
Alisema
mbali na Iringa, mikoa mingine 10 inayonufaika na mpango huo wa AFAP ni Njombe,
Ruvuma, Morogoro, Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Mbeya, Rukwa, Katavi na Kigoma.
Kwa
upande wake Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Iringa, Adam Swai aliishukuru
taasisi ya AFAP akisema ni matumaini yake itawasaidia wakulima kutatua kero ya
kucheleweshea mbolea.
“Wito
wangu niuelekeze kwa mawakala watakaofanya kazi na taasisi hii kuwa waaminifu
na kutoa ushirikiano ili mpango huu uweze kufanikiwa na hatimaye mipango ya
serikali na wakulima katika kuongeza tija katika kilimo ifanikiwe,” alisema.
Katika msimu wa 2014/2015, mawakala 25 waliothibitishwa kufanya kazi na AFAP watasambaza zaidi ya tani 96,000 za mbolea kwa wakulima wadogo zaidi ya Milioni 2 kupitia mtandao wa mawakala wadogo wa vijijini zaidi ya 1,060.
0 comments:
Post a Comment