Chama cha NCCR-Magezi kimesema, vigogo wote waliohusika kutoa na kupokea mgawo wa fedha kutoka akaunti ya Tegeta Escrow wafikishwe mahakamani akiwamo Mkurugenzi wa VIP Engineering Ltd, James Rugemalira .
Kashfa hiyo imesababisha Rais Jakaya Kikwete
kufanya mabadiliko madogo ya baraza lake la Mawaziri kutokana na
mawaziri wawili kujiuzulu.
Mawaziri waliotajwa kwenye sakata hilo ni Profesa
Anna Tibaijuka, ambaye alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi na aliyeingiziwa Sh1.6 bilioni na mwanahisa wa zamani wa Kampuni
ya IPTL, James Rugemarila.
Wengine waliopata mgao huo kutoka kwa Rugemarila
na kiasi katika mabano ni Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew
Chenge (Sh1.6 bilioni), Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja
(Sh40.4 milioni), aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel
Yona (Sh40.4 milioni), Mbunge wa zamani wa Sumbawanga (CCM), Paul Kimiti
(Sh40.4 milioni) na aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Tanesco, Dk Enos Bukuku
(Sh161.7 milioni).
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa
NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema waliofikishwa mahakamani hadi
sasa ni vidagaa lakini na vigogo mashuhuri wakiendelea kutamba.
“Mpokeaji na mtoaji wa rushwa wote ni wahalifu na
wanatakiwa kufikishwa mbele ya mahakama ili wajibu tuhuma
zinazowakabili...Rugenarila naye ni miongoni mwa watu wanaotakiwa
kufikishwa mahakamani.”
“NCCR tunataka kujua kwa nini baadhi waliopewa
rushwa wamefikishwa mahakamani lakini watu wengine kama Profesa
Tibaijuka, Chenge, Ngeleja, Yona, Kimiti na wengineo hawafikishwi
mahakamani? Wote wanatakiwa kwenda kujibu tuhuma zao,” alisema Nyambabe
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah alipotafutwa kuzungumzia kauli hiyo
ya NCCR alisema, “Sipo ofisini hivyo nisingependa kulizungumzia hilo.”
Waliofikishwa mahakamani hadi sasa ni Mhandisi
Mkuu wa Mradi wa Umeme Vijijini (Rea), Theophillo Bwakea na Mkurugenzi
wa Huduma za Kisheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Rugonzibwa Mujunangoma, ambao kwa pamoja wanadaiwa kupokea rushwa ya
Sh485.1 milioni.
Wengine ni Meneja Misamaha ya Kodi wa TRA,
Kyabukoba Leonard Mutabingwa, Mwanasheria Mwandamizi wa Tanesco, Steven
Roman Urassa na Mkurugenzi wa Fedha BoT, Julius Rutta Angello
wanaokabiliwa na mashtaka ya kuomba na kupokea rushwa ya jumla ya
Sh1.923 bilioni
0 comments:
Post a Comment