Makamanda wa OFM (katikati) wakiwa ndani ya benki.
WAKATI kukiwa
na dhana ya baadhi ya wafanyakazi na wateja wa mabenki nchini kuvujisha
taarifa za wateja wanaotoa kiasi kikubwa cha fedha kwa majambazi ambapo
mwishowe wateja hao huvamiwa na kuporwa, Oparesheni Fichua Maovu (OFM)
imetinga ndani ya benki kadhaa jijini Dar na kugundua udhaifu mkubwa
katika ulinzi, Ijumaa Wikienda limeshika ushahidi mkononi.
Kutokana na matukio mfululizo ya wateja kuvamiwa mara baada ya kutoka
kuchukua fedha ndani ya mabenki, watu kadhaa walitoa malalamiko yao kwa
OFM wakitaka suala hilo lifanyiwe kazi kwa kuwa wao wanaamini kuna
udhaifu mkubwa kwenye sekta ya ulinzi.
Wakizungumza na Ijumaa Wikienda kwa masharti ya kutotaja majina yao,
baadhi ya watu hao walisema wapo wafanyakazi au wateja ambao wanaweza
kuingia benki na kutoa taarifa za mteja mwingine ambaye anatoa pesa
nyingi kwani ulinzi ni mdogo.
MALALAMIKO
“Unajua
ukikuta mtu anaweza kuingia benki akaongea na simu akiwa kwenye foleni
ni tatizo. Siku hizi hata baadhi ya mabenki, hata wale wanaotoa huduma
(teller) nao wana uwezo wa kuwasiliana kwa simu huku kukiwa na wateja na
wao wakiwa kwenye madirisha yao.
“Tabia
hii ndiyo chanzo cha ujambazi mkubwa unaotokea siku hizi. Mtoa huduma
anaweza kumwambia jambazi nje kwa simu kwamba kuna mtu amevaa suti
anatoka na mkoba mweusi una milioni kumi kwa sababu yeye si ndiye
amemtolea?
“Au
wateja wanaoongea na simu wakiwa kwenye foleni, ni rahisi kuvujisha
taarifa kwa majambazi. Unajikuta unakwenda kuvamiwa mbele ya safari
kumbe watu walikufuatilia tangu ndani ya benki,” alisema mmoja wa watu
hao.
Mmoja wa makamanda wa OFM akiongea na simu bila kizuizi chochote kutoka kwa walinzi wa benki.
OFM YAINGIA KAZINI
Baada ya kupokea malalamiko hayo, OFM ilijipanga na kuanza kuzungukia benki mbalimbali jijini Dar ili kupata ukweli.
KAZI YAANZA
Januari
12, mwaka huu, saa 7:24 mchana, makamanda wa OFM walitinga ndani ya
benki moja kubwa iliyopo maeneo ya Mnazi Mmoja, Dar, mmoja akiwa na
bastola kibindoni huku mwingine akiwa na simu ya mkononi ambayo
aliitumia kuongea na watu kila mara bila kuchukuliwa hatua yoyote licha
ya kuwepo kwa matangazo yaliyosomeka; switch off your phone (zima simu
yako).
Kama hiyo haitoshi, makamanda waliokuwa na kibarua cha kuchukua picha ya
kile kilichokuwa kikiendelea ndani ya benki hiyo, walishuhudia wateja
wengine wakizungumza kwa simu kwa sauti za juu huku wenzao wakitoa fedha
bila kuhofia usalama wao.
SAA 7: 43 MCHANA
Bila
kutambulika, kamanda mmoja wa OFM alichukua simu yake ya mkononi na
kumpigia mwenzake aliyekuwa nje na kuzungumza naye kwa sekunde 33 kisha
kukata na kupiga tena ambapo alitumia sekunde 17 na kuendelea kuchati na
watu wengine bila kizuizi chochote.
Kamanda
mwingine aliyekuwa na bastola ndani ya mfuko alijaza fomu ya kuweka
fedha (deposit slip) na kwenda moja kwa moja kwa ‘teller’ kuweka fedha
zake.
Kamanda wa OFM akiwa na bastola ndani ya benki.
Hadi saa 8:02, makamanda wanaondoka kwenye benki hiyo, hakuna mhusika
hata mmoja aliyeshtukia zoezi hilo, jambo lililoonesha kuwa uvamizi
ndani ya benki au kuvuja kwa taarifa za wateja wanaohudumiwa ni rahisi
kuliko inavyoweza kudhaniwa.
BENKI YA PILI
Januari
17, mwaka huu, saa 5:16 asubuhi. makamanda wa OFM walitinga ndani ya
benki nyingine iliyopo maeneo ya Mwenge jijini Dar, zoezi likiwa kama
lile la awali ambapo kamanda mmoja wa OFM alibeba bastola na kujitoma
nayo ndani huku mwingine akiwa na simu ya mkononi.
Saa
5:17, kamanda wa OFM akiwa na bastola inayoonekana kuchomoza nje ya
mfuko wa suruali, aliingia ndani ya benki hiyo na kujaza fomu bila
kumjali mlinzi aliyekuwa pembeni.
Saa
5:19, kamanda akaelekea upande wa maulizo ambapo aliomba maelekezo ya
jinsi ya kufungua akaunti na kuambiwa asubiri kwa muda.
Dakika 7 baadaye, mhudumu wa maulizo alimwita kamanda na kumpa fomu yenye maelezo ya jinsi ya kufungua akaunti na kuondoka zake.
Saa 5:21
kamanda aliyekuwa na simu alimpigia mtu aliyekuwepo nje ya benki na
kuongea naye kwa dakika 2 huku hali ikiwa kama ile ya benki ya awali
ambapo hakukuwa na katazo lolote kutoka kwa mlinzi wa benki hiyo.
Timu
nzima ya OFM iliondoka maeneo hayo kwa mtindo wa kijasusi bila
kushtukiwa jambo ambalo kwa benki iliyojizatiti kwa ulinzi, makamanda wa
OFM wangeshtukiwa mapema.
LENGO LA OFM
Lengo la
OFM kufanya ushushu kuhusu madai ya udhaifu wa ulinzi kwenye baadhi ya
mabenki, si kuzisakama benki hizo bali kuwaondoa katika usingizi mzito
wa ulinzi kwani ujambazi kwa sasa jijini Dar hasa kwa wateja wanaotokea
benki ni jambo la kutisha.
Tayari gazeti hili lina mlolongo wa wateja waliopigwa risasi na kufa
wakiwa wanatoka ndani ya benki kuchukua fedha. Swali ni je, majambazi
hao huwa wanaambiwa na nani kwamba, mteja anayetoka amebeba ‘mzigo
mnono’?
Gazeti hili linamshauri Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova kusimamia suala hili kwa karibu ili kupunguza matukio ya
ujambazi katika benki.
0 comments:
Post a Comment