Home » » Ripoti ya CAG Yaanika 'Madudu' Kibao Serikalini

Ripoti ya CAG Yaanika 'Madudu' Kibao Serikalini

Wakati Rais John Magufuli akipambana dhidi ya ufisadi, uzembe na ukwepaji kodi na uovu mwingine dhidi ya mali za umma, ripoti mpya ya ukaguzi iliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inaonyesha ana kazi kubwa zaidi kupata ushindi kwenye vita hiyo. 

Ripoti hiyo ya mwaka 2014/ 2015 iliyowasilishwa bungeni jana na CAG Mussa Juma Assad imeibua uozo zaidi kwenye halmashauri, taasisi za Serikali na mashirika ya umma, ikibainisha kuwa nchi ina tatizo kubwa zaidi ya watu ambao wamekuwa wakishughulikiwa na Serikali ya Awamu ya Tano. 
 
Ripoti hiyo ya pili ya Professa Assad tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo mwaka juzi, imegusa taasisi zilizowahi kuwa chini ya Rais John Magufuli na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako na Balozi Asha Rose Migiro, ambaye alikuwa Waziri wa Sheria na Katiba. 
 
Ripoti hiyo pia inaonyesha ufisadi katika ununuzi na uingiaji mikataba uliofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), matumizi yasiyo ya lazima kwenye Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Afya, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jeshi la Wananchi, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi na mkoa wa Tabora. 
 
Pia ripoti hiyo imebainisha kuwa mapendekezo mengi ambayo CAG amekuwa akiyatoa kwa takribani miaka saba sasa, hayatekelezwi. 
 
Katika ripoti hiyo, CAG anaonyesha dosari kwenye utendaji wa Wakala wa Huduma za Ufundi na Umeme (Temesa), na Wakala wa Barabara (Tanroads), taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi ambayo wakati huo ilikuwa ikioongozwa na Dk Magufuli. 
 
Profesa Ndalichako alikuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), wakati NEC imeguswa na ripoti hiyo katika suala la mchakato wa kuandika Katiba upya ulioongozwa na Wizara ya Katiba na Sheria. 
 
Ripoti hiyo ya Profesa Assad pia imebainisha kuwa Deni la Taifa, ambalo hutokana na fedha zinazopowa kutoka ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kugharimia matumizi ya Serikali, limekuwa kwa tofauti ya Sh7 trilioni. 
 
Tangu aingie madarakani Novemba 5 mwaka jana, Dk Magufuli amekuwa akitumia ripoti zilizopita za CAG kusimamisha kazi au kutengua uteuzi wa watumishi wa umma wanaotuhumiwa kujihusisha na ufisadi, lakini amekuwa akikosolewa kuwa hajaweka mfumo wa kukabiliana na hali hiyo. 
 
Katika ripoti hiyo, CAG anasema Temesa ilinunua kivuko chenye kasi ndogo kuliko ilivyotarajiwa na hadi ulipokuwa unafanyika ukaguzi Agosti 2015, chombo hicho kilikuwa hakifanyi kazi kwa zaidi ya mwaka. 
 
“Kuhusu dosari katika ununuzi wa kivuko chenye thamani ya Sh7,916,955,000, Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Umeme, mitambo na ufundi (Temesa) iliingia mkatabana M/s Johs.Gram-Hanssen Bergensgade 10, DK 2100 Copenhagen Oe Denmark wa ununuzi wa kivuko cha Dar es Salaam –Bagamoyo chenye thamani ya Dola za Marekani 4,980,000 bila Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT),” anasema CAG. 
 
“Dosari zifuatazo zilibainika katika manunuzi hayo. Kasi ya kivuko haikuzingatia matakwa ya mnunuzi.  Ripoti ya mtaalamu wa ukaguzi ilibainisha kwamba kiwango cha juu na chini cha kasi ya kivuko wakati wa majaribio kilikuwa na kiwango kati ya knots 19.45 na knots 17.25 kinyume na makubaliano yaliyoainishwa kwenye mkataba wa kasi ya kiwango cha 20,” anafafanua.
 
“Pili kivuko kilikabidhiwa bila hati ya makabidhiano Novemba 17, 2014 baada ya ucheleweshwaji wa siku 16; Pia nilibaini kwamba mpaka wakati wa ukaguzi, Agosti 2015, hati ya makabidhiano ilikuwa haijatolewa na mzabuni.” 
Ununuzi wa feri hiyo uliwahi kuzua sakata bungeni huku wabunge wa upinzani wakilalamika kwamba kilikuwa bomu kwani kinatumia zaidi ya saa tatu kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo badala ya dakika 45 za gari. 
 
Eneo jingine lililoguswa na CAG ni la malipo yaliyofanywa na Tanroads kwa makandarasi waliomaliza kazi zao. Kwamba moja ya matatizo makubwa ya taasisi hiyo ni udhaifu katika menejimenti. 
 
“Wakala wa Barabara (Tanroads) iliingia mikataba mbalimbali ya ujenzi wa barabara na madaraja. 
 
"Wakati wa ukaguzi nilibaini kwamba baadhi ya mikataba haikukamilika kwa muda uliopangwa kutokana na kuchelewa kwa ulipaji wa fedha. 
  
"Pia, nilibaini kwamba ucheleweshwajiwa malipo ya kati ya mikataba 16 ulisababisha ulipaji wa riba kiasi cha Sh 5,616,652,022 na Dola za Marekani 686,174.86,” alisisitiza CAG. 
 
Profesa Assad amezungumzia pia ukaguzi maalumu alioufanya kuhakiki fedha zilizowahi kutolewa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa taasisi mbalimbali zilizoko chini yake. 
 
Ukaguzi huo ulifanywa kutokana na ombi lililowasilishwa na katibu wa Bunge kwa barua yenye Kumb. NaCBC.155/188/01/26 ya Desemba 19, 2013. 

Bunge lilitaka kujua kama fedha zilizotolewa na wizara hiyo kwenda idara na taasisi zilizo chini yake zilipokewa na kutumiwa na wahusika kama ilivyopangwa. 
 
Katika ukaguzi huo, CAG alibaini kasoro katika vitabu vya akaunti za fedha vya Necta mwaka 2010, Sekretarieti ya Elimu ya Jumuiya ya Madola, Chuo Kikuu Huria (OUT), na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (Adem). 
 
“Udanganyifu wa malipo ya Sh185,350,000 yaliyolipwa Necta. Aprili 2010 kiasi cha 185,350,000 kilitumwa Necta kama matumizi ya kawaida. Wakati wa ukaguzi ilibainika kuwa kiasi hiki cha fedha hakikuandikwa kwenye vitabu vya uhasibu vya Necta. Hata hivyo, ilibainika kuwa stakabadhi ya mapokezi ya fedha hizo iliyotolewa na watumishi wasio waaminifu wa Necta ilikuwa ya kugushi,” anasema. 
 
“Kuhusu fedha zilizopelekwa OUT ni kwamba kati ya mwaka 2009/2010 Wizara ilihamisha Sh90,000,000 kwenda Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola, ni kiasi cha Sh40,734,000 ambacho kilipokewa huku Sh49,266,000 hakijulikani. 
 
“Pia katika mwaka wa fedha 2010/2011 Wizara ilipeleka OUT Sh10,486,252,913 lakini ni Sh10,427,109,020 tu zinazoonekana kwenye vitabu huku Sh59,143,893 zikiwa hazimo kwenye vitabu.” 

Vilevile, CAG amesema katika ukaguzi huo Sh188, 838,528 zilizopelekwa Adem mwaka 2009/2010 zimeyeyuka. Mwaka huo Wizara ilipeleka Sh712,798,788 kwa taasisi hiyo, lakini vitabu vinaonyesha Sh523,960,260 zilipokewa na kurekodiwa, huku Sh188, 838,528 zikikosekana kwenye vitabu. 
 
Mbali ya CAG kuonyesha madudu katika matumizi ya fedha, pia ameonyesha matumizi mabaya ya Sh7,080 milioni katika mchakato wa uchapaji Katiba Inayopendekezwa.
Facebook Blogger Plugin: Bloggerized by Joseph Kipangula Enhanced by Joseph Kipangula

0 comments:

Post a Comment

NURU FM 93.5 IRINGA

.

.

.

Nyali

Pages

Pages

Powered by Blogger.

Blog Archive

Search This Blog