Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla amekumbana na joto la Mbeya baada ya
meya wa jiji hilo, Mchungaji David Mwashilindi na madiwani wake 34
kususia kikao chake cha kujitambulisha kwa wananchi, baada ya kudaiwa
kwenda kukagua Soko la Mwanjelwa bila kumpa taarifa yoyote meya wa jiji
hilo.
Meya alifikia uamuzi huo ndani ya ukumbi wa Mkapa muda
mfupi kabla ya Makalla kuanza kuzungumza na watumishi wa jiji, wananchi,
wazee maarufu, viongozi wa dini na machifu ambapo Mkuu wa Wilaya ya
Mbeya Nyirembe Sabi alimkaribisha Meya Mwashilindi kuzungumza chochote
kwa niaba ya madiwani wake.
Hata hivyo, Meya Mwashilindi
alipochukua kipaza sauti alisema: “Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, nakumbuka kwa
mara ya kwanza kukutana na wewe tulizungumza kwamba tufanye kazi, siasa
zimekwisha. Lakini masikitiko yangu ni kwamba leo hii umekwenda Soko la
Mwanjelwa bila ya mimi mwenye jiji kupewa taarifa yoyote wala madiwani
wangu. Sasa hiki kikao hakinihusu hivyo muendelee na kikao chenu.”
Baada
ya kusema maneno hayo alikabidhi kipaza sauti kwa mkuu wa wilaya, kisha
akachukua nyaraka zake akainuka pamoja na madiwani wote kupitia Chadema
na kutoka ukumbini huku wakisikika wakisema, ‘hizi ni siasa ambazo
tulizikataa, lakini wanatulazimisha kuendesha siasa. Hatuwezi kupuuzwa
kwa kiasi hiki.”
Mkuu wa Wilaya, Mnasa alisema anaamini taratibu
na ratiba yote ilipangwa vizuri hivyo hawaoni sababu ya madai ya
madiwani hao kwamba hawakushirikishwa kwenye ziara hiyo, wao kama
wawakilishi wa Rais hawaangalii siasa, bali wanaangalia uchapakazi na
siyo masuala ya siasa.
Akizungumzia kitendo cha meya na madiwani
wake kususia kikao hicho, Makalla alisema ‘Nashangazwa na uamuzi wa
madiwani hawa kwa kitendo hiki, kwani siku ile nilipotembelea Shule ya
Sekondari Iyunga, nilisema kwamba Aprili 20 ambayo ndiyo leo (jana)
nitakuwa na ziara ya jiji na kabla ya kikao nitataka kutembelea Soko la
Mwanjelwa,” alisema Makalla.
Alisema suala la meya na madiwani
wake kutoshirikishwa kwenye ziara ya kwenda Soko la Mwanjelwa halimhusu,
kwani mwenye wajibu wa kupeana taarifa ni kwenye ngazi ya halmashauri
ya jiji, lakini siyo yeye (Makalla).
0 comments:
Post a Comment