Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete ameahirisha kwa muda kwenda
bungeni mjini Dodoma, kufuatia kuungua moto kwa mabweni ya Shule ya
Sekondari Bwilingu.
Akizungumza shuleni hapo juzi jioni,
Ridhiwani alisema katika vipaumbele vyake elimu ni mojawapo, hivyo
hawezi kuondoka na kuwaacha wanafunzi waliounguliwa vifaa wakishika tama
na wengine kushindwa kuhudhuria darasani kwa kukosa nguo na madaftari.
Alisema
moto ni kitu cha dharura na kwa kutambua hivyo, amewasiliana na wadau
mbalimbali na wahisani ambao wameamua kulivunja jengo lililoungua na
kulijenga upya, kazi iliyoanza jana.
Ridhiwani alisema
wamechangia misaada mbalimbali ikiwamo magodoro, vitanda, nguo, vyombo,
madaftari, sabuni, vyandarua, mafuta, dawa ya mswaki na miswaki kwa
wanafunzi hao.
“Unajua moto ulitokea usiku, sasa muda huo ina
maana hao wanafunzi 65 walikuwa na kalamu moja na daftari moja au mawili
wanajisomea darasani, vingine vyote vilikuwa mabwenini na vimeungua,”
alisema.
“Kwa hiyo nimeona bora nishirikiane na wenzangu kutatua
hili na nimetoa tayari magodoro 70 na mashuka 140 na nguo kadhaa waanze
navyo, huku vingine vikifuata baadaye.”
Mkuu wa sekondari hiyo,
Emmanuel Kahabi alisema pamoja na kupata maafa hayo, jana wanafunzi
waliendelea na masomo kama kawaida kwa kuwa baada ya tukio, wadau
mbalimbali walikutana na kuanza kutoa misaada.
Moto huo ulitokea
Jumapili usiku na kuteketeza vifaa na mali zote zilizokuwa ndani wakati
wanafunzi wakiwa kwenye masomo ya usiku madarasani.
0 comments:
Post a Comment