Watumishi
15 wa Idara za Ardhi, Mipango Miji na Ujenzi katika Manispaa ya Bukoba
mkoani Kagera akiwemo Msanifu wa Majengo wa Manispaa hiyo, Abukar Issa,
wanashikiliwa na Polisi kwa uchunguzi zaidi dhidi ya tuhuma za kugawa
hati ya ardhi kinyume cha Sheria ya Ardhi ya Mwaka 2004.
Agizo
la kuwakamata watumishi hao limetolewa na Mkuu wa Mkoa, John Mongella
kutokana na kikao cha dharura alichokiitisha ofisini kwake baina yake na
watumishi hao wa idara hizo.
Mongella
alisema amewaita ofisini kwake watumishi wote kutoka idara za Ardhi,
Mipango Miji na Ujenzi kutaka kujua ni nani alitoa kibali kwa mmiliki wa
kiwanja hicho kilichopewa namba 09 L kinachopatikana katika Barabara ya
Uganda mjini Bukoba, huku watumishi hao wakionekana kutupiana mpira.
Alisema
watumishi hao walikuwa wakitambua kuwa kiwanja husika kipo katika
hifadhi ya Mto Kanoni ambao umekuwa ukiathiriwa na ujenzi holela na
kuhatarisha uchafuzi wa mazingira katika Ziwa Victoria.
Kiwanja
hicho ambacho kiliguswa na safishasafisha ya Desemba 9, mwaka huu siku
ya maadhimisho ya Uhuru ambayo katika mkoa huo yaliambatana na usafi na
uondoshaji wa makazi yaliyo ndani ya mita 60 kutoka katika hifadhi ya
mto Kanoni unaopeleka maji yake ndani ya Ziwa Victoria.
Ofisa
Mipango Miji wa Manispaa ya Bukoba, Catres Rwegasira naye alikuwa na
maswali ya kujibu mbele ya Katibu Tawala wa Mkoa huo, Nassor Mnambila na
Mkuu wa Mkoa huo.
Rwegasira
alisema kwa mujibu wa sheria mpya ya ardhi ya mwaka 2004, hairuhusiwi
mtu yeyote kuendesha shughuli wala kuweka jengo katika eneo hilo la mto
ndani ya mita 60.
Naye
Ofisa Msanifu wa Majengo, Abubakar Issa alipohojiwa na mkuu huyo wa
mkoa kuhusu nani alitoa kibali cha ujenzi katika kiwanja hicho wakati
wakijua kuwa ni makosa; Issa alikubali kuwa yeye ndiye alihusika.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Manispaa ya Bukoba, Aron Kagulumjuri alisema Manispaa hiyo
ilikwishapiga marufuku ujenzi katika kiwanja hicho kinachopakana na mto
huo, lakini hajui ni namna gani taratibu zilikiukwa.
Mkuu
wa mkoa alisema watumishi hao 15 wamechukuliwa na kupelekwa katika
Kituo Kikuu cha Polisi mjini Bukoba kwa uchunguzi zaidi na endapo yeyote
atabainika na shtaka kujibu hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa.
0 comments:
Post a Comment