Kasi
ya Rais John Magufuli ya kutumbua majipu serikalini inatarajiwa
kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM), mara tu atakapokabidhiwa rungu la
uenyekiti na Mwenyekiti wa chama hicho kwa sasa, Rais mstaafu, Jakaya
Kikwete.
Mara
tu atakapokabidhiwa rungu la uenyekiti, Magufuli anatarajiwa kufanya
kile kile anachoendelea kukifanya ndani ya serikali kwa kuwaumbua
viongozi ndani ya chama hicho waliojigeuza miungu watu na wanaoharibu
taswira ya chama.
Habari
za ndani zinasema kuna viongozi ndani ya chama hicho ambao
wamejimilikisha na wamekuwa wakineemeka na miradi mbalimbali ya chama
hicho huku chama kikitegemea ruzuku ya serikali pekee kujiendesha.
Katibu
wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, aliandika jana katika ukurasa wake
wa Twitter kwamba baada ya kumaliza serikalini mabadiliko yatahamia
kwenye chama.
“Tunachotaka kuwaambia wananchi ni kuwa baada ya kumaliza serikalini mabadiliko yatahamia kwenye chama,” aliandika kwenye ukurasa wake
Mmoja wa viongozi wandamizi ndani ya CCM amedokeza kuwa Magufuli anatarajia kutembeza fagio la chuma atakapokabidhiwa uenyekiti ili kurudisha heshima ya chama hicho kwa jamii.
Alisema
hivi sasa wafanyabiashara wengi na matajiri wamekimbilia CCM na wengine
kutumia mamilioni ya fedha kutafuta vyeo ikiwa ni ujanja ujanja wa
kuficha maovu yao.
“Hivi
sasa kama huna fedha usijisumbue kugombea nafasi ndani ya chama maana
hutapata kitu, chama ni kama kimegeuka cha matajiri maskini hawana chao
tena sasa Magufuli hatapenda kuona hali hii ikiendelea kuna watu lazima
watakwenda na maji,” alisema kiongozi mmoja
“Imefikia
wakati watu wenye tuhuma mbalimbali za ufisadi na wengine wakituhumiwa
kwa kufadhili vikundi vya ujambazi wanawania kuteuliwa na chama kugombea
nafasi mbalimbali ndani ya chama ….ndiyo maana wananchi wakakichoka
chama sasa, Rais Magufuli kwenye kampeni zake za urais alibaini hilo na
lazima atembeze fagio la chuma,” alisema kiongozi huyo.
Imekuwa
kawaida kwa Mwenyekiti wa CCM kumwachia nafasi hiyo Rais aliyeko
madarakani hata kabla ya muda wa uchaguzi ndani ya chama hicho
haujafika.
Rais
mstaafu wa awamu ya pili, Alhaji Hassan Mwinyi, alimwachia, Benjamin
Mkapa nayeye Mkapa alimwachia, Jakaya Kikwete mwaka 2006.
Kama
utaratibu huo utaendelea watu wengi wanatarajia, Mwenyekiti wa sasa wa
CCM, Kikwete atamkabidhi nafasi ya uenyekiti John Magufuli mwakani.
0 comments:
Post a Comment