Mkuu wa Jeshi La Polisi Nchini (IGP), Ernest Mangu Apiga Marufuku Vyama Vya Siasa Kuwa na Vikundi Vya Ulinzi
INSPEKTA Generali wa Polisi (IGP), Ernest Mangu amepiga marufuku vikundi vya ulinzi vya vyama vya siasa ambavyo vina muonekano na muundo wa vyombo vya usalama, kwani ni kinyume cha katiba na sheria ya nchi.
Vilevile, amevitaka vyama hivyo kuhakikisha vinafuata muongozo uliotolewa na Ofisi ya Msajili wa vyama hivyo na kama vikienda kinyume jeshi litapambana navyo.
Mangu alitoa tamko hilo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Jeshi la Polisi uliokuwa ukijadili namna ya kuondoa vikundi hivyo au namna ya kuboresha shughuli za uendeshwaji wa vikundi hivyo.
Alisema wamejadiliana na vyama hivyo na kwamba ofisi ya msajili imetoa muongozo ambao wanatakiwa kufuata katika kutekeleza ili waweze kufanya kazi zao kwa utaratibu unaotakiwa.
IGP Mangu alisema Katiba na sheria za nchi haziruhusu vikundi hivyo kuwepo, kwani jukumu la kulinda raia na mali zao ni la Jeshi la Polisi, hivyo vinaingilia kazi ya jeshi hilo.
“Katika mkutano huu tumekubaliana kuwa vyama vinatakiwa kufuata muongozo kutoka Ofisi ya Msajili na kama watashindwa kufanya hivyo basi sisi jeshi tuko tayari kupambana nao,”alisema IGP Mangu.
Mangu alisema mkutano huo utawasaidia kupata uelewa pole pole lakini kinachotakiwa hadi kufikia wakati wa uchaguzi mkuu vikundi vyote visiwepo.
Alisema suala la chama kuwa na vikundi vya vijana vyenye misingi ambayo haivunji Katiba ya nchi ni sahihi lakini kinyume cha hapo hawezi kuvumilia hali hiyo.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Peter Mziray alisema kuna vyama ambavyo vimekuwa na vikundi vya ulinzi na kuvitaja kuwa ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Wananchi (CUF).
Mziray alisema historia inaonesha kuwa vikundi hivyo vilikuwa wakati wa chama kimoja hivyo kinachoonekana sasa ni vikundi hivyo kufanya kazi ya Polisi jambo ambalo ni kinyume cha taratibu, sheria za nchi na katiba.
Alisema uwepo wa vikundi hivyo ni kinyume cha sheria hivyo katika mkutano huo wanajaribu kuviangalia kama uendeshwaji wa vikundi hivyo kama ni sahihi au si sahihi.
“Unajua vikundi hivi vipo miaka mingi tatizo ni wakati huu vinaonekana kuwa na mitizamo tofauti jambo ambalo linahatarisha usalama wa nchi,” alisema Mziray.
Mziray alisema vyama vya siasa vinatakiwa kufuata mapendekezo yaliyotolewa kama wakishindwa jeshi litashughulika nalo.
Mbali na hayo, alisema katika mkutano huo vyama viwili ambavyo ni Chadema na CUF havikuhudhuria lakini ujumbe utawafikia na watatakiwa kutekeleza.
Aidha, Mziray alilitaka Jeshi la Polisi kusimamia misingi ya sheria katika utekelezaji wa majukumu yake kwani kinyume cha hapo ndipo migogoro inaibuka kila kukicha.
Mziray alisema kitendo cha katiba za vyama vyao kubainisha vikundi hivyo na msajili kuvikubalia isiwe ni sababu ya kuruhusu migongano hiyo. Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ally Vuai alisema wao hawana vikundi vya ulinzi ndani ya chama.
Alisema kuwa vijana wao hawawaandai kijeshi ila kuwa vijana bora kiitikadi na kuwa na mwamko wa kujua siasa.
“Sisi hatuwafundishi kuwa magaidi ila tunawafundisha kuwa vijana bora ila kuna muonekano wa mavazi ambao jeshi wakiona wanaweza kutia shaka, lakini kama tatizo ndiyo hilo tunaweza kurekebisha,” alisema Vuai.
Kwa upande wake, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi aliwataka viongozi wa vyama kusoma sheria za nchi na kuzielewa ili wasizivunje kwa kisingizio cha kujilinda.
Mutungi alisema ofisi yake itahakikisha inawapatia elimu viongozi wa vyama ili kuhakikisha wanatambua mipaka yao ya kisheria katika kuunda vikundi hivyo.
Msajili huyo alisema ni jukumu la vyama na Jeshi la Polisi kujipanga na kukaa pamoja ili waweze kufikia muafaka kuhusu changamoto ambazo zinawakuta na si kuingia kwenye migongano.
“Unajua kinachotokea hapa ni kukosekana kwa uaminifu katika pande hizi mbili lakini wakati wa kutambua kuwa katiba na sheria za nchi zinataka nini ni huu ili kuepuka migogoro,” alisema.
CUF yanena
Naibu Mkurugenzi Habari na Uenezi wa CUF, Abdul Kambaya, alisema hawawezi kufuta kikundi chao cha ulinzi (Blue Brigade) kwani kinatumika kulinda ulinzi wa mali za chama na viongozi wake.
“Polisi wenyewe wanalalamika hawatoshi kutoa ulinzi kwa wananchi wote, lakini pia sisi kama CUF hatuwezi kuacha kutoa ulinzi mathalan kwa mwenyekiti wetu, Profesa Ibrahim Lipumba. Na hili limo kwenye katiba yetu.
“Kikundi hiki hakipo kupambana na watu, na kama kuna mahali kimefanya kosa kichukuliwe hatua…kwanza uamuzi uliofikiwa ni wa kidikteta kwani hatujashirikishwa,” alisema Kambaya.
Chadema
Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe alisema kikundi chake cha ulinzi cha Red Brigade kitaendelea kuwepo hadi pale haki itakapotendeka.
Alisema lengo la kikundi chao cha ulinzi ni kulinda viongozi, mali za chama na wanachama wao katika mikutano kwani Jeshi la Polisi limeshindwa kuwajali Chadema na kuegemea upande wa CCM.
Mbowe aliongeza inaonekana hiyo ni hofu ya uchaguzi mkuu hasa kwa kuzingatia matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Desemba 14, mwaka jana, upinzani umeshinda maeneo mengi.
Alisema kuwa Jaji Mutungi ana uwezo wa kufuta vikundi hivyo kwa mamlaka aliyonayo, lakini hawezi kufuta yaliyoko moyoni kwa watu katika kujilinda.
“Haki ikitendeka katika mchakato mzima wa uchaguzi kwa siasa za Tanzania, hakutakuwa na sababu ya kuwa na vikundi hivyo.
“Leo (jana), tumezindua mafunzo ya vijana wa Chadema yanayohusu ulinzi na usalama ambapo uzinduzi utaendelea kufanyika kila mahali,” alisema Mbowe na kuongeza kama polisi wamejitosheleza kwa nini kuna polisi jamii.
Mbowe alisema hawakuonekana kwenye kikao hicho kwa sababu ya majukumu mengine ya kichama nje ya Dar es Salaam.
Credit:Jambo Leo
0 comments:
Post a Comment