MKE ACHINJWA KISA KWENDA SALUNI NA KUPENDEZESHWA, MAJIRANI WADAI ASINGEKUFA MKE ANGEKUFA MUME.. SIMULIZI YAO INASIKITISHA.
Enzi za uhai wake, Mary Lucas (20) anaedaiwa kuchinjwa na mumewe.
Tukio hilo lililoacha
simulizi ya kushangaza miongoni mwa wanandoa na wanaotarajia kuingia,
lilijiri Aprili 18, mwaka huu nyumbani kwa mwanaume huyo, Mtaa wa
Mapinduzi ‘A’ Kata ya Duga jijini hapa.
WANACHOKIJUA POLISI WA TANGA
Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Tanga, ACP Zuberi Mwombeki alitangaza kwa waandishi wa habari kwamba,
mauaji hayo yalitokea saa nne na nusu asubuhi ya Aprili 18 mwaka huu.
Alisema chanzo cha tukio
hilo ni wivu wa kimapenzi kati ya wawili hao ambapo marehemu alimuomba
mumewe pesa kiasi cha shilingi elfu kumi aende saluni kutengeneza
nywele lakini mwanaume akasema hana.
“Mwanaume hakumpa pesa
marehemu lakini baadaye alimkuta amesuka na ndipo ugomvi ulipoanzia hapo
hadi kutokea mauaji hayo,” alieleza kamanda huyo.
UWAZI LAANZA NA MAJIRANI
Mengi yamesemwa kufuatia
mauaji hayo, lakini kama kawaida ya Gazeti la Uwazi ni kufuatilia kwa
kina ili kujua chanzo cha kila habari inayotakiwa kuandikwa gazetini.
Ili kujua nini kilitokea
kabla na baada ya mauaji hayo, Uwazi lilizungumza na baadhi ya majirani
wa nyumbani kwa mtuhumiwa huyo ambaye kwa sasa anashikiliwa na polisi
chini ya ulinzi mkali.
“Jamani sisi wenyewe
tumeshtuka sana kwa kifo cha Mary, mimi nimeongea naye akiwa anakwenda
saluni na hata aliporudi. Kama angejua ndiyo siku yake ya kufa naamini
asingekwenda. Inauma sana!
“Mary alitoka saluni
akiwa amependeza maana alitengenezwa nywele vizuri sana. Mimi mwenyewe
nilimsifia. Kufika nyumbani kwake, mzozo ukaanza.
“Mumewe alitaka kujua
alikotoa shilingi elfu kumi ya kuendea saluni maana yeye hakumpa. Mzozo
ulikwenda hadi mwanaume akachukua panga na kumchinja. Naamini ni wivu,”
alisema jirani mmoja.
KUMBE WALIKUWA NA HISTORIA YA UGOMVI
Jirani mwingine, Shaban
Juma yeye alisema: “Hawa watu wameishi katika hali ya kutoelewana na
walikuwa wakigombana kila wakati, lakini hatukujua kama litatokea hili
kwani mara zote katika kugombana kwao, mwanaume ndiye aliyekuwa akipigwa
jambo ambalo liliwafanya watu wa karibu yake kumshauri kuvunja
uhusiano wao kulikoni aibu ya kupigwa na mke.”
Jennifer Charles yeye
pia ni jirani, alisema: “Siku ya tukio Mary alimwomba mumewe hela ya
kwenda kutengeneza nywele saluni lakini mume hakuwa na pesa siku hiyo
lakini baada ya kuondoka nyumbani, marehemu naye alikwenda saluni.
“Baadaye mume aliporudi
nyumbani hakumkuta Mary lakini mara alirudi akiwa ametengenezwa nywele
jambo lililomfanya bwana kuhisi kuwa fedha hizo amehongwa na mwanaume
mwingine tofauti na yeye na hivyo kuzuka ugomvi huo.”
MUME ALITOKA NJE AKITAMBA KUUA
Baada ya Jennifer
kumaliza kusimulia hayo, Juma Ally, naye ni jirani, akaendeleza:
“Hatukujua kilichoendelea katika mzozo wao, lakini baadaye ukimya
ulitawala. Muda mfupi mbele mume alitoka nje na kutuambia kwamba
ameshaua huko ndani kwani amechoka kupigwa na sasa amejibu mapigo.
“Kwanza tulijua anatutania lakini tulivyoona kimya kimezidi tukaamua kuingia ndipo
tulipomkuta marehemu
akiwa chini, akitoka damu nyingi. Tuliogopa kwa kweli. Mary mrembo
tunayemjua sisi, amelala chini na damu chapachapa.
“Alikuwa ana majeraha
makubwa sehemu ya shingo na kichwani yaliyotokana na kupigwa na panga.
Ilionekana panga lilikuwa kali sana na panga lenyewe lilikuwa pembeni
yake. Ndipo tulipoamua kumkimbiza Hospitali ya Mkoa, Bombo ambapo
alipoteza maisha wakati madaktari wakihangaika kuokoa uhai wake.”
ASINGEKUFA MKE
Naye, Fatuma Ramadhani
alisema kutokana na ugomvi wa mara kwa mara kati ya wawili hao na
mwanaume kupigwa kila wakati, majirani waliamini siku moja mume huyo
ndiye angekuja kupata madhara hata kufa kutokana na alivyokuwa akipigwa.
MTUHUMIWA KUPANDA MAHAKAMANI WAKATI WOWOTE
Kamanda Mwombeki alisema upelelezi unaendelea ili kuweza kumfikisha mahakamani mtuhumiwa huyo.
Marehemu Mary alizikwa katika eneo la Mwakizaro jijini Tanga, siku ya pili baada ya tukio hilo la kuhuzunisha.
0 comments:
Post a Comment