Tuesday , November 5, 2013
‘Hatujafuta alama sifuri matokeo ya mitihani’
Na Sharon Sauwa, Mwananchi
Dodoma.Naibu
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, amesema Serikali
haijafuta daraja sifuri katika matokeo ya mitihani taifa ya shule za
sekondari na kwamba ilichokifanya ni kuondoa mrundikano wa madaraja.
Mulugo aliyasema hayo jana bungeni, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Catherine Magige (CCM).
Magige alitaka kufahamu kama kushusha madaraja ni suluhisho la kuwaokoa
vijana waliofanya vibaya katika mitihani ya kidato cha nne mwaka jana.
Mapema katika swali lake la msingi, Magige, alitaka kufahamu kama
Serikali ina mkakati wa kuanzisha mpango maalumu hasa wa ufundi kwa
wanafunzi waliofanya vibaya katika mitihani ya kidato cha nne mwaka
jana.
Akijibu swali hilo, Mulugo alisema hawajashusha madaraja wala kuweka viwango tofauti na ilivyokuwa awali.
“Tumeongeza madaraja ili kuwatambua watoto, kulikuwa na mrundikano
katika daraja moja. Serikali haijafuta division ziro na wala hakuna
division V, ipo division I, II,III, IV na ziro kama kawaida,” alisema.
Alisema uamuzi wa kushusha madaraja, hauna lengo la kuwaokoa wanafunzi
wanaofanya vibaya na badala yake, unalenga katika kuondoa mrundikano wa
alama katika daraja moja.
Alitoa mfano wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), kuwa lilikuwa linapanga daraja F kuanzia alama 0 hadi 34.
Alisema kulikuwa hakuna ufuatiliaji wa maendeleo ya mwanafunzi kama
kanuni inavyosema kuwa lazima kuwe na ufuatiliaji wa asilimia 50 kwa 50 .
Alisema kanuni hiyo inataka kutunzwa kwa alama 50 katika ufuatiliaji wa
maendeleo ya mwanafunzi na katika mtihani ya kumaliza shule asilimia 50.
Alisema wameanza kuyaweka madaraja kwa kutofautiana kwa alama 10 kila daraja.
Alisema bado daraja la ufaulu litaendelea kuwa 40 ama alama C.
Hata hivyo, baada ya kumaliza kujibu swali hilo, Spika wa Bunge, Anne
Makinda, aliiagiza Serikali kupeleka bungeni kauli ya waziri kuhusiana
na suala hilo.
“Naibu Waziri nenda mtuletee kauli ya Serikali kuhusiana na utaratibu huo ili kupata majibu yanayoridhisha,” alisema
Kuhusu wanafunzi waliofanya vibaya mwaka jana katika mitihani yao,
Mulugo alisema Serikali haitaanzisha mpango maalumu wa ufundi kwa vijana
hao.
Alisema badala yake, Serikali inawashauri wazazi kuwashawishi watoto kurudia mtihani wa kidato cha nne.
Kwa mujibu wa Mulugo, kwa mwaka huu, jumla ya watahiniwa 60,507 wa kujitegemea wamejisajili kufanya mtihani wa kidato hicho.
Lowassa: Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa hauna meno
Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam/Dodoma.Waziri
Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa amesema ana shaka kama Mpango wa
Matokeo Makubwa Sasa (Big Result Now), utafanikiwa kutokana na Kitengo
cha Utekelezaji, Ufuatiliaji na Tathmini ya Miradi ya Maendeleo kilicho
chini ya Ofisi ya Rais (PDB) kukosa meno.
Akichangia mjadala wa hoja ya Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa
Taifa wa mwaka 2014/2015, Lowassa alisema tatizo kubwa linaloikabili
nchi ni viongozi kushindwa kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo.
“Tatizo la nchi hii mnazungumza mambo mengi lakini hakuna utekelezaji,”
alisema Lowassa wakati akichangia mjadala huo uliowasilishwa na Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira, wiki
iliyopita.
Mbunge huyo wa Monduli (CCM), Lowassa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati
ya Bunge Mambo ya Nje alisema itakuwa vigumu kwa PDB kutekeleza wajibu
wake wakati hakina meno ya kusimamia utekelezaji wa mipango ya Serikali.
Kitengo cha PDB kinachoongozwa na Omar Issa kiliundwa mwaka huu na
kutengewa kiasi cha Sh29 bilioni na kulalamikiwa na Mbunge wa Ubungo
(Chadema), John Mnyika wakati wa kikao cha Bunge cha Bajeti 2013/14.
Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuinua
uchumi kutoka wa chini hadi kufikia wa kati ifikapo mwaka 2025.
“Nataka mjiulize maswali machache. Je, hawa PDB wana meno?” alisema Lowassa na kuongeza:
“Tunazungumza lakini mjue kuwa `discipline’ (nidhamu) ya wenzetu wa
Malaysia ni tofauti na hapa kwetu. Hapa kuna uswahili mwingi wa kukaa
bila kutekeleza mambo, mnaamua bila kutekeleza.” Huku akishangiliwa na
baadhi ya wabunge, Lowassa aliitaka Serikali kuwa na mipango michache
ambayo itakayoweza kuifuatilia kwa ukaribu na kuitekeleza. Alipendekeza
kuwa ajira, elimu na kuendeleza reli kuwa vipaumbele muhimu.
“Kinatakiwa chombo ambacho kinaweza kufanya uamuzi mgumu unaotekelezeka
kwelikweli. Bila kuwavika joho la kufanya uamuzi ili kuwarahisishia
utekelezaji wa kazi yao na wakawa na ‘function’ itakuwa ni kazi bure. Ni
uamuzi mzuri kuanzisha mpango huu lakini msipoangalia itakuwa kazi
bure. Lazima wawe na meno ya kuuma mkishakubaliana mambo yafanyike.”
Kila mtu analalamika
Lowassa alisema sasa Tanzania imekuwa nchi ya kila mtu kulalamika, kuanzia viongozi hadi wananchi.
“Wananchi na viongozi wote wanalalamika haiwezekani kukawa na jamii ya
aina hii, lazima awepo mtu mmoja anayefanya uamuzi na anayechukua hatua.
Bila kuchukua hatua tutaendelea kulalamikiana tu” alisema.Mpango
wa Matokeo Makubwa uliingizwa nchini kwa kurudufiwa kutoka Malaysia,
ambayo ilipopata uhuru mwaka 1957 ilikuwa katika kiwango sawa na
Tanzania katika maendeleo ya kiuchumi lakini sasa ina rekodi ya juu
kiuchumi barani Asia. Mpango huu pia unatekelezwa Nigeria na Rwanda na
umeonyesha mafanikio makubwa katika nchi hizo.
Katika kutekeleza mpango huo, Serikali imeanza na wizara sita; Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Kilimo, Chakula na Ushirika, Maji, Uchukuzi, Fedha na
Nishati na Madini.
Ajira
Akizungumzia suala la elimu, Lowassa alisema: “Huwezi kuzungumza mipango
bila kuzungumza ajira, kuna Watanzania wengi waliomaliza darasa la
saba, kidato cha nne na sita wapo mitaani na hawana ajira. Tusipoangalia
watakuja kula sahani moja na sisi.”
Alisema katika mkutano wa Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha
Duniani (IMF) mwaka huu, walizungumzia mdororo wa uchumi kwa nchi za
Ulaya na moja ya nchi hizo ambayo ni Hispania, ilieleza jinsi ilivyoweza
kujinasua kwa kuweka kipaumbele cha ajira.
“Hispania walitoa mfano kuwa walikuwa na ukosefu wa ajira kwa asilimia
50, waliamua katika bajeti yao kujikita katika kuzalisha ajira. Kila
mwekezaji aliyekwenda katika nchi hiyo alipewa masharti ya kuwekeza
katika ajira ya vijana. Kimsingi tunatakiwa kuwa na takwimu za kujua
tumezalisha ajira ngapi ndipo tutajua uchumi wetu unakua kwa kiasi
gani,” alisema.
Lowassa alisema baada ya miaka mitatu nchi hiyo imetoka kuwa miongoni
mwa nchi zisizo na ajira na kusisitiza kuwa mipango mingine ni migumu
kutekelezeka kama nchi haitakuwa na ajira.
Alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatma Mwasa na Mkuu wa Wilaya ya
Igunga, Elibariki Kingu kutokana na kitendo chao cha kuwapa ajira
wanafunzi waliohitimu vyuo vikuu baada ya kuwapatia matrekta na
mashamba.
Elimu
Lowassa alisema kuna tatizo la msingi katika elimu ya Tanzania.
“Nilitegemea wahusika wangepata taarifa ya Tume ya Serikali kuchunguza
kushuka kwa kiwango cha elimu ili kujua matatizo yaliyopo katika elimu
na nini cha kufanya.”Mwanzoni
mwa mwaka huu Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliunda tume ya watu 15
kuchunguza sababu za idadi kubwa ya wanafunzi wa kidato cha nne
kuvurunda katika matokeo ya mtihani huo mwaka 2012.
Tume hiyo tayari imeshakamilisha kazi na kukabidhi ripoti hiyo serikalini, lakini mpaka sasa bado haijawekwa hadharani.
“Haitoshi kumchukua mwanafunzi aliyemaliza chuo kikuu wakati akienda
katika soko la ajira wakati shahada yake hamsaidii, mtu ana shahada
lakini kazi hakuna.”
“... Kunatakiwa kufanyika mjadala nchi nzima kuzungumza juu ya matatizo
na nini kifanyike. Nchi isipokuwa makini katika hili itaachwa katika
ushindani uliopo sasa kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na nchi
wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).”
Awafagilia Magufuli, Mwakyembe
Akizungumzia uendelezaji wa Reli ya Kati alisema pamoja na juhudi
zinazofanywa na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli kujenga barabara,
alisema zinaharibika kwa kasi kutokana na kuzidi kwa kiwango cha uzito
wa malori.
“Reli ya Kati inatakiwa kuangaliwa kwa haraka maana malori yanayotembea
katika barabara yatapungua kwa kuwa mizigo itakuwa inachukuliwa na
treni,” alisema. Licha ya kusifu kazi inayofanywa na Waziri wa Uchukuzi,
Dk Harrison Mwakyembe Lowassa alisema foleni jijini Dar es Salaam
zinashusha uzalishaji, kwani watu wengi wanatumia muda mwingi barabarani
kuliko kufanya shughuli za maendeleo.
“Serikali haiwezi kukaa hivi hivi, ‘this is a disaster’ (hili ni janga),
mtafute njia ya kuangalia mnafanyaje kumaliza foleni ya Dar es Salaam,
jambo hili lifanyike sasa,” alisema.
Uamuzi mgumu
Lowassa alisema pia Tanzania haitakiwi kuendelea kulumbana na Uganda,
Rwanda na Kenya zinazotaka kuitenga katika Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC), badala yake ichukue uamuzi mgumu wa kushirikiana na nchi
nyingine.
“Wao wameamua kuanzisha ushirikiano na Sudan Kusini, Tanzania inaweza
kuanzisha ushirikiano na Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo (DRC) ambako ni
kuzuri zaidi na kikubwa kinachotakiwa kufanyika ni kuifufua Reli ya
Kati,” alisema.
Mapigano mapya yazuka DRC
Mapigano makali yamezuka kati ya majeshi ya serikali ya Congo na waasi wa M23 katika mpaka wa mashariki na taifa la Uganda.
Mapigano makali yameripotiwa kutokea wakati majeshi hayo ya serikali
yanapojaribu kuchukua udhibiti wa maeneo yaliosalia mikononi mwa waasi
wa M23.
Waasi wa M23 mnamo siku ya Jumapili
walitoa wito kwa wapiganaji wao kusitisha vita ili kuruhusu mazungumzo
ya amani kufanyika kati ya viongozi wa kundi hilo na waasi hao.Mwandishi
wa BBC Issac Mumena aliyeko katika eneo hilo la mpaka wa Uganda na DRC
anasema kuwa mapigano hayo yamesababisha maelfu ya wakimbizi kuvuka na
kuingia nchini Uganda kutafuta usalama na matibabu kwa wale
waliojeruhiwa.
Hata hivyo, kwa mujibu mwa mwandishi wa BBC hakuna dalili ya kufanyika mazungumzo ya amani.
Anasema kuwa hali ni tete sana katika eneo la mpakani.
Inaarifiwa kuwa waasi hao wanaonekana kujibu vikali mashambulizi makali
kutoka kwa wanajeshi wa serikali na hali ni mbaya kuliko siku za awali,
na taarifa zinasema kuwa wanajeshi wanakaribia kushinda vita vyao dhidi
ya waasi hao.
Mapigano ya hivi sasa yanakuja baada ya wanajeshi wa serikali kudhibiti
baadhi ya miji iliyokuwa imetekwa na waasi hao baada ya kuwafurusha.
TRA Yapata Gari lenye mbambo Scana wa Kukagulia Makontena Bandarini Zenj.
Gari Maalum lenye mtambo wa kukagulia makontena kujuwa thamani ya mzingo
ulioko katika kontena baada ya kupitishwa katika mtambo huu unaotumia
Scana kuona kilichomo ndani ya kontena, bila ya kufunguliwa kama
ilivyokuwa hapo nyuma makontena hukaguliwa kwa kufunguliwa na kutizama
kila kilichomo ndani. Mtambo huu utasaidia baadhi ya wafanyabiashara
ambao hudangaya na kuandika bidhaa tafauti na ziliomokatika kontena na
kuisababishia Serekali kukosa mapoto kutokana ushuru wa bidhaa
zinazoingizwa Zanzibar.
Likiwa katika sehemu yake maalum ya kukagulia makontena katika bandari
ya Zanzibar kama linavyonekana pichani likisubiri kufanya kazi yake
Washukiwa wa ugaidi mahakamani Kenya
Wanaume wanne wamefikishwa mahakamani nchini Kenya baada ya kuhusishwa
na shambulizi la kigaidi lililofanyika dhidi ya jengo la Westgate nchini
Kenya mwezi Septemba.
Wanne hao wote walikanusha mashitaka hayo ikiwemo kosa la kuingia nchini
bila vibali halali pamoja na kumiliki stakabadhi bandia za
kujitambulisha.
Mahakama imeamuru wawekwe rumande.
Kundi la kigaidi la Somalia, Al Shabaab lilikiri kufanya shambulizi hilo la kigaidi ambapo zaidi ya watu sitini waliuawa.
Wanne hao walishitakiwa kwa kosa la kuhusika na shambulizi hilo la
kigaidi ingawa hakuna hata mmoja alikuwemo ndani ya Jengo la Westgate
wakati wa shambulizi hilo.
Wanne hao raia wa Somalia ni Mohammed Ahmed Abdi, Liban Abdullah, Adan Adan na Hussein Hassan.
Washukiwa hao ambao hawakuwa na mawakili walizuiliwa rumande kwa wiki
moja baada ya kiongozi wa mashitaka kuomba muda zaidi kufanya uchunguzi.
Sunday, November 3, 2013
Wapinga kuahirishwa kesi ya Kenyatta
Waathirika wa kesi inayomkabili rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta wameutaka
Umoja wa Mataifa kukataa wito wa kutaka kucheleweshwa kwa kesi dhidi ya
Rais Kenyatta katika mahakama ya kimataifa ya ICC mjini The Hague,
Uholanzi.
Baadhi ya viongozi wa Afrika wameandaa rasimu ya azimio la kuomba kesi
inayomkabili Rais Kenyatta iahirishwe kwa mwaka mmoja kwa masilahi ya
usalama wa taifa, kufuatia shambulio la kigaidi katika kituo cha
kibiashara cha Westgate mjini Nairobi.
Lakini mwanasheria wa waathirika, Fergal Gaynor, amesema kucheleweshwa
kwa kesi kutapunguza nafasi ya kupatikana haki kwa waathirika. Bwana
Kenyatta anakanusha mashitaka yanayomkabili dhidi ya uhalifu wa
kibinadamu, kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007.
Tusiache siasa ichague mfumo wa elimu
Na Mwananchi
Kwa muda mrefu sekta ya elimu nchini imepitia mabadiliko mengi, pia
kuzua hoja na maswali mengi yakiwamo ya siasa kuachwa itawale mfumo wa
utoaji elimu katika nchi yetu.
Hali kadhalika, sekta hii imekutana na changamoto lukuki, zikiwamo
malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali ambao wamekuwa wakieleza kwamba
elimu yetu inashuka kwa kiwango cha kutisha.
Hadi sasa zimetolewa sababu nyingi za kuporomoka kwa kiwango hiki cha
elimu katika Tanzania katika miaka ya karibuni ambazo zinahusisha pande
mbalimbali. Pande hizo ni pamoja na walimu, wanafunzi, wazazi au walezi,
mazingira ya kujifunzia na kufundishia ambayo ni pamoja na madarasa,
maabara, vitabu, ukosefu wa motisha hasa kwa walimu, utoro wa wanafunzi,
mimba na kadhalika.
Ikumbukwe kuwa katika miaka ya karibuni ukiwamo mwaka jana, tumeshuhudia
kushindwa vibaya kwa wanafunzi wetu waliohitimu kidato cha nne.
Matokeo hayo mabaya yaliiduwaza, kuilazimisha Serikali kuyafuta, kutaka
usahihishaji, upangaji matokeo ufanyike upya na yote yalifanyika.
Kutokana na hilo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa niaba ya Serikali aliunda tume maalumu ili kuchunguza na kubaini kilichotokea.
Miongoni mwa kazi za tume ile zilikuwa ni kuchunguza na kubaini upungufu
wote uliotokea na kisha kupendekeza ni hatua gani zinafaa kuchukuliwa.
Hata hivyo, ripoti ya tume hiyo ambayo iliongozwa na Profesa Sifuni
Mchome, Katibu Mkuu wa sasa wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
haijatolewa hadharani.
Ripoti hiyo imekuwa hata hivyo ikinukuliwa na vyombo vya habari ikionyesha upungufu mwingi katika elimu nchini.
Hali ikiwa bado ni hivyo, wiki hii, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
imetangaza mfumo mpya wa kutoa matokeo ya kidato cha nne na sita ambao
utaanzia na wahitimu wa kidato cha nne ambao wanaanza mitihani yao
kesho.
Uamuzi huo ambao umetangazwa na Profesa Mchome tayari umezua maswali
mengi kutoka kwa wadau wakihoji kama kweli unalenga katika kuinua au
kuporomosha zaidi kiwango cha elimu.
Wengine wameukosoa mfumo huo kwamba umefanyika zaidi kisiasa, unalenga
katika kuwafurahisha wakubwa, hauna uhalisia na mazingira halisi ya
elimu katika nchi yetu.Nasi,
kama wadau wa elimu nchini bado tunajiuliza ni wapi tuendako katika
mipango yetu ya elimu na endapo mfumo huo utakuwa mwarobaini wa
kuondokana na matokeo mabaya katika mitihani kwa vijana wetu, upungufu
ambao umekuwa ukiendelea nchini katika miaka ya karibuni.
Tunaamini, mabadiliko haya katika mfumo huo wa mtihani ambayo
yanahusisha maendeleo ya mwanafunzi darasani, mtihani wa kidato cha
pili, mihula kwa kidato cha tatu na nne, unaweza kuwa mzuri, lakini
unahitaji kufanyiwa utafiti zaidi.
Wasiwasi wa wengi likiwamo Baraza la Taifa la Mitihani (Necta) ni kwamba
baadhi ya walimu si makini katika kuandaa na kutuma maendeleo ya kila
siku ya wanafunzi wao, kwa hali hiyo huenda tukafaulisha hata wale
wasiostahili.
Tunaungana na wadau hao kuamini kuwa Tanzania inajichimbia kaburi katika
elimu kwani mbele ya safari itakuwa na wahitimu wengi lakini wasiokuwa
na uelewa wa kutosha, wasioweza kushindana na wenzao kutoka nchi jirani
za ukanda huu wa Afrika Mashariki.
Kwa maana hiyo, tunashauri wadau na wizara wakutane, wauangalie kwa
umakini mfumo huu mpya ambao ukichukuliwa kama mzaha unaweza kuwa kaburi
letu kielimu.
Tunasema kama nchi hatujachelewa, lakini lazima kila mmoja akubali
kutimiza wajibu wake katika kuhakikisha tunakuwa na wahitimu
walioandaliwa vizuri na kuiva, walimu wanaofanya kazi kwa moyo, uzalendo
wala si kwa kuangalia mitihani, bali mtalaa wa elimu, mafunzo katika
nchi yetu.
0 comments:
Post a Comment