WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amesema ni muhimu kwa Tanzania
kukimbia kwa kasi ili kukabiliana na changamoto za maendeleo ya
kisanyansi duniani.
Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli (CCM), aliyasema hayo jana
alipokuwa akihutubia katika sherehe za Jubilee ya miaka 25 ya uaskofu na
miaka 40 ya upadri ya Askofu Paul Ruzoka wa Jimbo Kuu Katoliki la
Tabora.
Kwa mujibu wa Lowassa, elimu ya Tanzania inakabiliwa na changamoto
nyingi na kwamba njia sahihi ya kukabiliana na changamoto hizo ni kwenda
na kasi ya maendeleo duniani.
“Ni wazi kwamba, mabadiliko haya makubwa yametufikisha mahali ambako
sisi kama taifa tunapaswa kuchukua hatua za kuruka ili kuweza
kukabiliana na kasi kubwa ya maendeleo yanayotokea duniani hivi sasa.
“Maendeleo hayo makubwa yanapaswa yawe darasa la kuirejesha Tanzania
katika falsafa ya elimu ya kujitegemea kwani elimu hiyo inajenga misingi
imara kwa wahitimu wanaomaliza shule na vyuo kuanzia kidato cha nne na
kuendelea ili waweze kujiajiri au kuajiriwa katika sekta mbalimbali,”
alisisitiza Lowassa.
Pamoja na hayo, Lowassa ambaye amekuwa mdau wa elimu nchini,
alilipongeza Kanisa Katoliki kwa mchango mkubwa linaoutoa katika
maendeleo ya elimu nchini.
Alisema kwamba, kanisa hilo limekuwa mstari wa mbele katika kusaidia
kujenga misingi imara ya kupambana na maadui wakubwa wa maisha ya
binadamu wakiwamo ujinga, umasikini na maradhi.
Pia, aliliomba kanisa hilo lishirikiane na Serikali na wananchi
katika ulinzi na usalama kwa kuwa kuna dalili za kuvurugika kwa amani
baada ya uwepo wa matukio ya ugaidi nchini.
Pia, Lowassa alimuomba Askofu Ruzoka aendelee kusaidia kutatua
matatizo katika nchi za maziwa makuu zikiwamo Burundi ambako pameanza
kuchafuka.
Awali, Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Mhashamu Askofu
Tarcius Ngalalekumtwa, alimpongeza Askofu Ruzoka kwa kazi kubwa
aliyoifanya katika kipindi cha miaka 25 ya uaskofu.
“Baba Askofu nakupongeza sana kwa mengi uliyoyafanya hususani kule
Burundi ambako umesaidia kuleta amani na leo hii tunaye baba askofu
kutoka Burundi,” alisema Askofu Ngalalekumtwa.
0 comments:
Post a Comment