Serikali wilayani hapa Mkoa wa Geita,
imepiga marufuku walimu kuvaa mavazi yasiyolingana na taaluma yao na
upakaji wanja na rangi ya mdomo kupita kiasi wanapokuwa kazini.
Ofisa Utumishi wa Wilaya ya Geita, Thabitha Bugema alitoa amri hiyo
leo wakati akizungumza na walimu wakuu wa shule za msingi na waratibu
elimu kwenye kikao cha muongozo wa kutumia fedha za elimu bure
zilizotolewa na Serikali.
Bugema alisema baadhi ya walimu wanavaa mavazi ya upotoshaji ambayo hayaendani na ya ofisini.
Alisema walimu wa kiume huvaa suruali za jeans, fulana zenye nembo ya
timu za mpira na wengine kuvaa mlegezo na kunyoa nywele mitindo isiyo
ya heshima.
“Nashindwa kuelewa wapo walimu wanavaa kama wauza baa, amejipaka
lipstick (rangi ya mdomo) na wanja kama anakwenda kwenye kumbi za muziki
usiku, wakuu wa shule sitegemei kuwaona mkifumbia macho walimu wa aina
hiyo,” alisema Bugema
Alisema kila mtumishi wa Serikali anafahamu mavazi ya ofisini na
kuwataka walimu kubadilika na kuvaa mavazi ya heshima yanayoendana na
taaluma yao.
Ofisa Elimu Msingi Wilaya ya Geita, Deus Seif alisema wamepokea Sh80
milioni kwa ajili ya elimu bure na kuwataka wakuu wa shule kuhakikisha
zinatumika kama ilivyopangwa.
Mkuu wa wilaya hiyo, Manzie Mangochie
aliwataka walimu na waratibu elimu kufanya mikutano ya wazazi ya
kuwaelimisha maana ya elimu bure na kuwaeleza mambo ambayo Serikali
inafanya na wajibu wa wazazi kwa watoto wao.
0 comments:
Post a Comment