KATIKA kukabiliana na madereva wa
pikipiki wanaopakia abiria zaidi ya mmoja maarufu mshikaki, Jeshi la
Polisi mkoani Pwani litatumia mbinu mpya ya kuwapiga picha madereva hao
na kuwakamata baadaye wakiwa kwenye vituo vyao.
Jeshi hilo litatumia mbinu hiyo ili
kuepusha ukamataji kwa kuwakimbiza wale wanaofanya hivyo kwa lengo la
kuepuka kusababisha ajali wakati wa kuwakamata madereva hao wanaobeba
mshikaki.
Akizungumza na waandishi wa habari
ofisini kwake mjini Kibaha, Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Bonaventura
Mushongi alisema kuwa mbinu hiyo itasaidia kuwabaini na kuwapiga faini
kwa mujibu wa sheria.
“Tumeona tufanye hivyo kwani ukamataji
wa zamani wa kufukuzana siyo mzuri, unaweza ukasababisha ajali kwa
wanaotumia pikipiki hiyo na hata kugonga watu au mali katika kukwepa
mkono wa sheria lakini kwa kuwapiga picha tutawatafuta na kuwakamata
wakiwa hawana abiria,” alisema.
Alisema mbali ya kukamata madereva
bodaboda wanaobeba mshikaki ambayo ni kinyume cha sheria, pia
watawakamata kwa makosa mengine kama vile leseni, kutokuwa na kofia
mbili ngumu na kutozingatia sheria za uendeshaji na usalama barabarani.
“Pia tunawaomba waendesha bodaboda
watupe ushirikiano katika kubaini wahalifu ambao wamekuwa wakitumia
usafiri huo kufanikisha wizi hivyo wanapaswa kutupa taarifa za watu
wanaopanga kwenda kufanya uhalifu kutumia vyombo hivyo,” alisema
Mushongi.
Aidha alisema kuwa endapo madereva hao
wa bodaboda watatoa ushirikiano kwa polisi itasaidia sana kukabiliana na
uhalifu ambao umekuwa ukijitokeza mara kwa mara.
“Pia kuna taarifa kuwa
baadhi ya waendesha bodaboda nao wanajihusisha na uhalifu, tunawataka
waache vitendo hivyo kwani wao ni watoa huduma na endapo watabainika
kufanya hivyo watakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria,” alisema Mushongi.
Alibainisha kuwa jeshi lake
litashirikiana na viongozi wa bodaboda katika kuhakikisha kuwa wanafuata
sheria na kupambana na uhalifu na siyo wao kuwa chanzo cha uhalifu na
kuvunja sheria.
0 comments:
Post a Comment