Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba
Maadhimisho ya Sherehe za kutimia Miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya
mwaka 1964 yatafanyika kama kawaida na kupangwa kuanza rasmi leo
jumapili ya Tarehe 3 Januri 2016.
Alisema
Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha kwamba katika muda wote wa
maandamisho hayo kunakuwa na hali ya utulivu na usalama mkubwa katika
maeneo yote ya Visiwa vya vya Unguja na Pemba.
Balozi
Seif Ali Iddi ambae pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Maadhimisho ya
Kitaifa Zanzibar alisema hayo wakati akitoa Taarifa rasmi ya ratiba ya
maadhimisho ya sherehe za Miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar mbele ya
Wana Habari hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema
suala la upande wa Upinzani kuzisusia sherehe za Mapinduzi kwa
kisingizio cha Rais aliyepo madarakani si halali ni muendelezo wa
kuwapotosha Wananchi walio wengi nchini.
Balozi
Seif alifafanua kuwa Rais wa sasa Dr. Ali Mohammed Shein ataendelea
kuwa rais hadi yule atakayechaguliwa rasmi na kihalali na Wananchi ale
kiapo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kama
ilivyokwishatolewa ufafanuzi na wanasheria walio wengi.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Miradi yote ya Maendeleo
ipatayo 24 ambapo 16 ikiwa imekamilika na Minane inatarajiwa kuwekwa
mawe ya msingi imehusishwa katika maadhimisho hayo itakayoanza Jumatatu
ijayo.
Alisema
madhimisho hayo yataanza rasmi leo Jumapili ikiwa ni siku maalum kwa
kazi za usafishaji wa masingira katika maeneo mbali mbali Unguja na
Pemba ukilenga zaidi katika sehemu za kutolea huduma za kijamii kama
Hospitali, Vituo vya Afya pamoja na masoko.
Mwenyekiti
huyo wa Halmashauri ya Maadhimisho ya Kitaifa Zanzibar alifahamisha
kwamba ingawa zoezi hilo hufanyika kila zinapoanza sherehe za Mapinduzi
lakini mwaka huu juhudi malum zinapaswa kuchukuliwa ili kuhakikisha
maeneo yote yanakuwa katika hali ya usafi muda wote.
Akigusia
suala la hatma ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar ambalo limekuwa agenda
kubwa kwa baadhi ya watu wakiwemo hata wanasiasa nchini wakiendelea
kupotosha Wananchi Balozi Seif alisema Taarifa rasmi ya vikao
vinavyowakutanisha Viongozi wa juu kulijadili suala hilo itatolewa rasmi
mara baada ya kukamilika kwa mazungumzo hayo.
Hata
hivyo Balozi Seif alitanabahisha kwamba Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar {
ZEC } kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ndio yenye mamlaka
ya kuendesha na kusimamia uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.
Alisema
kwa vile tume hiyo kupitia Mwenyekiti wake haikuridhika na mazingira
yaliyojichomoza wakati wa zoezi la kupiga kura na kulazimika kufuta
Uchaguzi pamoja na matokeo yake yote Taasisi hiyo hiyo ndio yenye uwezo
wa kuitisha uchaguzi mwengine kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar.
Akijibu
baadhi ya maswali ya Waandishi wa Habari Balozi Seif alisema katiba ya
Zanzibar ya Mwaka 1984 iko wazi na kutoa mamlaka kwa tume ya uchaguzi ya
Zanzibar kupanga uchaguzi mwengine kufuatia kufutwa kwa ule wa mwezi
oktoba mwaka 2015.
0 comments:
Post a Comment