Kambi ya Upinzani imelizidi maarifa Bunge na kurejesha sakata la kuuzwa
nyumba za Serikali ambalo juzi lilisababisha kiti cha Spika kuagiza
yaondolewe maneno yanayomtaja Rais katika hotuba ya maoni mbadala.
Juzi, Kamati ya Kanuni za Bunge ilihariri hotuba ya msemaji wa kambi ya upinzani wa Wizara ya Mambo ya Ndani, ikiondoa maneno yanayomtaja Rais John Magufuli na badala yake kuweka neno Serikali kwenye sakata la uuzwaji nyumba za Serikali.
Juzi, Kamati ya Kanuni za Bunge ilihariri hotuba ya msemaji wa kambi ya upinzani wa Wizara ya Mambo ya Ndani, ikiondoa maneno yanayomtaja Rais John Magufuli na badala yake kuweka neno Serikali kwenye sakata la uuzwaji nyumba za Serikali.
Kamati hiyo pia iliondoa suala la
mkataba wa Jeshi la Polisi na kampuni ya Lugumi Enterprises, rushwa,
mauaji ya wanasiasa, mwenendo wa Rais na Bunge kulinda wahalifu, jambo
lililomfanya msemaji wa kambi hiyo, Godbless Lema kukataa kusoma hotuba
yake.
Lakini jana katika hotuba ya kambi ya upinzani kwa Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, mbunge wa Vunjo, James Mbatia
alilirejesha sakata hilo akieleza kuwa ni muda sahihi kwa Rais John
Magufuli kurekebisha kasoro zilizojitokeza wakati akiwa waziri ili
kurejesha imani katika jamii.
Mbali na sakata hilo, pia Mbatia
alizungumzia sakata la kivuko cha Mv Dar es Salaam ambacho kinatakiwa
kifanye safari kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo, akikielezea kuwa “ni
jipu ambalo limeiva kwa viwango vyote na sasa linatakiwa litumbuliwe
mara moja”.
Suala la Mv Dar es Salaam liliungwa mkono na Mbunge
wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe wakati akichangia hotuba ya
bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Zitto
alisema kuwa hoja ya kivuko hicho lazima ichukuliwe hatua ili iaminike
kuwa kuna nia ya dhati ya kupambana na ufisadi nchini.
“Naona suala hili linakwepwakwepwa, hivyo litolewe maamuzi,” alisema Zitto.
Pia
mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini alisema suala la Mv Dar es
Salaam kuwa iko chini ya kiwango, liliwahi kusemwa na mbunge wa upinzani
lakini Serikali ikakataa.
Hata hivyo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Serikali (CAG) amesema ukweli katika ripoti yake. “Hili suala inabidi
liangaliwe kwa kuwa kuna watu wanahitaji kutumbuliwa hivyo hao watu
waangaliwe,” alisema Selasini.
Akisoma hotuba ya maoni mbadala
ya kambi ya upinzani, Mbatia alisema wakala wa majengo nchini ndiye
muhusika mkuu katika kuhakikisha nyumba za Serikali zinakuwa katika hali
nzuri kwa watumishi wa Serikali kuishi.
“Katika muktadha huo,
kambi ya upinzania inalikumbusha Bunge kwamba kati ya mwaka 2002 mpaka
2004 Serikali iliuza nyumba 7,921 na mpaka mwaka 2008 ilikuwa imejenga
nyumba 650 tu,” alisema Mbatia.
Alisema katika biashara hiyo ya
kuuza nyumba zilizokuwa mali ya Tamisemi, Serikali ilipata Sh252 milioni
lakini sasa inahitaji kusaka zaidi ya mara mbili ya kiasi hicho kujenga
nyumba za fidia.
Mbatia alisema Serikali ingetumia Sh677.6 milioni kujenga nyumba mpya ili zirejeshwe Tamisemi.
“Kwa
vile hata wale waliouziwa nyumba hizo, kuna taarifa kati yao wapo
walioziuza na kujipatia faida kubwa kinyume na mikataba ya mauzo hayo,
kambi ya upinzani inapendekeza wanyang’anywe nyumba hizo kwa kukiuka
mikataba na malengo ya mauzo.”
Mbatia alisema kumbukumbu rasmi
za Bunge zinaonyesha Serikali ilitoa taarifa kuwa kamati iliundwa
kuchunguza mchakato wa mauzo ya nyumba hizo na ilitarajiwa kumaliza kazi
Februari 2007, lakini hadi leo hakuna taarifa iliyotolewa na Serikali
na kuitaka Serikali ya Awamu ya Tano izirejeshe.
Akinukuu
kumbukumbu rasmi za Bunge za Aprili 25, 2008 wakati wa kikao cha 18 cha
Mkutano wa 11, Mbatia alisema baada ya mjadala mkubwa wa hoja binafsi
iliyowasilishwa na mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro, Bunge kwa kauli moja
lilipitisha azimio kuwa nyumba hizo zirejeshwe serikalini.
“Bunge
linaazimia kwamba Serikali ifanye yafuatayo: Itekeleze mara moja bila
kusita, agizo la Rais kurejesha nyumba zilizouzwa kinyume cha utaratibu
na kwa watu ambao hawakuwa watumishi wa Serikali wakati huo na vilevile
nyumba ambazo hazikupaswa kuuzwa kama zile zilizopo kwenye maeneo ya
utawala wa Serikali,” alisema akinukuu azimio hilo.
Mbatia
aliitaka Serikali itafsiri kaulimbiu ya “hapa kazi tu” kwa kuelekeza
azimio hilo, akisema Kikwete alikosa uthubutu wa kusimamia msimamo wake.
“Tunajua uuzwaji huo ulisimamiwa na wizara aliyokuwa akiiongoza
yeye (Rais Magufuli) na kuna uwezekano mkubwa kwamba alisimamia maamuzi
ambayo hakuwa na uwezo wa kuyakiuka,” alisema Mbatia.
“Sasa ni muda sahihi Rais Magufuli kurekebisha kasoro alizozisimamia katika mchakato huo ili kurejesha imani katika jamii.”
Kivuko cha Bagamoyo
Kuhusu kivuko cha Bagamoyo, Mbatia alisema kilinunuliwa na Temesa chini ya uongozi wa Waziri wa Ujenzi wa Serikali ya Awamu ya Nne ambaye ndiye Rais wa sasa.
Kuhusu kivuko cha Bagamoyo, Mbatia alisema kilinunuliwa na Temesa chini ya uongozi wa Waziri wa Ujenzi wa Serikali ya Awamu ya Nne ambaye ndiye Rais wa sasa.
Mbatia alisema kwa mujibu wa
ripoti ya CAG katika hesabu za Serikali Kuu za mwaka ulioishia Juni 30,
2015 iliyotolewa Machi 2016, alibaini ununuzi wa boti ‘feki’ na mbovu
uliofanywa na Temesa na kugharimu dola 4,980,000 za Marekani (sawa na
Sh7.9 bilioni).
Alisema CAG alibaini masuala makuu mawili ambayo
ni kasi ya kivuko hicho ni tofauti na kasi iliyotakiwa kuwapo na pia
cheti cha kukikubali kivuko hicho kilikuwa kinyume na Kanuni ya 247 ya
Sheria ya Manunuzi ya Umma.
“Tabibu wa kutumbua jipu hili yuko wapi? Au msemo usemao kuwa ‘mganga hajigangi’ unatumika hapa?” alihoji.
Juzi
jioni hali kama hiyo ya kuzungumza masuala yaliyozuiwa na Kamati ya
Kanuni za Bunge, ilijitokeza wakati wabunge wakijadili Hotuba ya
Makadirio na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani.
0 comments:
Post a Comment