Wakati uchunguzi wa kampuni ya Lugumi inayodaiwa kushindwa kutekeleza
mradi wa utambuzi wa vidole kwenye vituo vya polisi ukiendelea, Baraza
la Vijana la Chadema (Bavicha) limemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya
nchi, Charles Kitwanga kujiuzulu wadhifa wake kupisha uchunguzi huo.
Limesema
haiwezekani waziri anayetajwa kuhusika katika sakata hilo kuendelea na
kazi huku Jeshi la Polisi linalodaiwa kutapeliwa na kampuni hiyo likiwa
chini ya wizara yake.
Hata hivyo, waziri huyo amewajibu vijana
hao wa upinzani kwa kusema hawezi kubishana na watoto na hayo
waliyoyatoa ni mawazo yao binafsi wana haki ya kuyasema.
“Nimeshasema mara nyingi, siwezi kuzungumza tena kuhusu haya mambo. Wao kama wamesema waache waseme,” alisema.
Baraza
hilo lililoibuka na hoja tatu jana, limesema kama waziri huyo atagoma
kujiuzulu kupisha uchunguzi unaofanywa na kamati ndogo ya Bunge ya
Hesabu za Serikali (PAC), Rais John Magufuli anapaswa kumwajibisha
ingawa suala hilo ni gumu kutokana na uswahiba uliopo kati ya kiongozi
huyo mkuu wa nchi na Kitwanga.
Kampuni ya Lugumi ilibainika
kutotimiza matakwa ya mkataba wake baada ya kufunga mashine 14 tu kati
ya 108 zilizotakiwa kufungwa, licha ya kulipwa zaidi ya asilimia 90 ya
fedha kwa mujibu wa mkataba ambazo ni Sh37 bilioni.
Ripoti ya
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2013/14
ndiyo iliyofichua udhaifu huo na baadaye Bunge kuanza uchunguzi baada ya
kutoridhishwa na maelezo ya Wizara ya Mambo ya Ndani na polisi kuhusu
mkataba huo.
0 comments:
Post a Comment