Silaha
ya kivita aina ya SMG na risasi 30 mali ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani
vimekutwa vimefichwa kwenye kichaka jirani na Mto Kitame katika Kata ya
Makurunge wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.
Silaha
hiyo inadaiwa iliibiwa kwenye Geti la Gama saa tisa usiku Desemba 24,
mwaka jana wakati askari wa hifadhi hiyo, Jackson Shirima (23) akiwa
kazini.
Kamanda
wa Polisi mkoani humo, Bonaventura Mushongi alisema jana kuwa tukio
hilo lilitokea muda mfupi baada ya askari huyo kutoka zamu ya lindo la
geti hilo na kujipumzisha kwenye moja ya mahema akiwa na silaha hiyo.
“Huyu
askari alikuwa zamu na kama ilivyo ada huwa wanapokezana zamu ya ulinzi
hivyo alitoka na silaha yake akaenda kujipumzisha kwenye hema maana
hifadhini hutumia mahema na alipitiwa na usingizi na ndipo ilipoibiwa na
mtuhumiwa aliyewahi kuwa mtumishi wa hifadhi hiyo,” alisema.
Mushongi alibainisha kuwa baada ya wizi huo, askari kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) walianza
msako na kupitia taarifa ya msamaria mwema walimkamata mtuhumiwa huyo,
mkazi wa Tegeta Kibaoni ambaye alikwenda kuonyesha alipokuwa ameificha
kichakani ikiwa na risasi 30.
Mkuu
wa hifadhi hiyo, Dk James Wakibara alisema wameshtushwa na tukio hilo
kwani halijawahi kutokea na kwamba, zaidi ni baada ya kukuta mtuhumiwa
huyo aliwahi kuwa mtumishi wao na aliacha kazi miezi kadhaa iliyopita
yeye mwenyewe.
Dk Wakibara alilishukuru Jeshi la Polisi kwa ushirikiano lilioutoa toka siku ilipoibiwa silaha hiyo hadi ilipopatikana.
0 comments:
Post a Comment