Matukio
ya ajali za barabarani yameendelea kuutikisa Mkoa wa Singida baada ya
abiria 10 kupoteza maisha na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa ndani ya
siku tisa.
Desemba
30, mwaka jana katika Kijiji cha Tumuli Wilaya ya Iramba abiria watatu
walikufa na wengine 25 kujeruhiwa na ajali nyingine ilitokea Januari
Mosi katika Kijiji cha Kintukuntu wilaya humo na kuua abiria mmoja na
kujeruhi watatu.
Ajali nyingine iliyohusisha bajaji ilitokea jana Januari 7 katika Barabara ya Mwankoko na kumuua dereva na abiria wawili.
Siku
moja kabla ya tukio hilo, ajali ya basi la Mohammed Trans lililokuwa
linatokea Tanga kwenda Shinyanga ilisababisha vifo vya abiria watatu na
kujeruhi wengine watano wote wakiwa ni walimu.
Akitoa
taarifa ya ajali ya basi la Mohammed Trans jana, Kaimu Kamanda Polisi
mkoani hapa, Mayala Towo alisema ilitokea Januari 6, saa nne usiku
katika Kijiji cha Mseko wilayani Iramba.
Kamanda
huyo aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Mussa Rajabu (55), Farahan
Manyama (34) na John Tungaraza (39) wote wakiwa ni walimu, wakazi wa
Geita.
Pia, alisema majeruhi ambao pia ni walimu wamelazwa katika hospitali ya wilaya hiyo.
Kamanda
huyo aliongeza kuwa walimu hao walikuwa wametokea kwenye Chuo cha
Eckenford mkoani Tanga walikokuwa wakichukua mafunzo mbalimbali. Alisema
chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva.
Towo
alisema basi hilo lenye namba za usajili T 786 AWJ aina ya Scania
lilikuwa linaendeshwa na Jovin Jackson (38), mkazi wa Shinyanga
liligonga kwa nyuma lori lenye namba B.6705A lililokuwa likivuta tela
B.0568A lililokuwa likienda Burundi.
Akifafanua,
alisema dereva wa basi alitaka kulipitia lori hilo, lakini alipogundua
hataweza aliamua kurudi ghafla kushoto na mwendo kasi aliokuwa nao
alijikuta analigonga lori hilo kwa nyuma.
Towo
alisema baada ya kusababisha ajali hiyo dereva alitoroka na kukimbilia
kusikojulikana. Juhudi zinaendelea kumsaka ili afikishwe mahakamani.
0 comments:
Post a Comment