Mara kwa mara kwenye jiji la Dar es Salaam, yamekuwa yakiandaliwa matamasha mbalimbali ikiwemo la Krismasi na Pasaka chini ya kampuni ya Msama Promotions. Lakini kwa wakati huu kilio cha wananchi kimesikika, hasa baada ya kampuni hii kuamua kupeleka tamasha la Krismasi kwa mwaka 2014 kwenye mikoa ya Mbeya, Iringa na Ruvuma. Haya yote ni kuanzia tarehe 25 ndani ya jiji la Mbeya, na kisha kuelekea Iringa tarehe 26 kabla ya kumalizia na Songea iliyopo mkoa wa Ruvuma tarehe 28 Disemba 2014.
Kwaya Maalum kuzindua Mbeya
Kwaya maalum jijini Mbeya wiki iliyopita iliingia kambini kwa siku moja kujiandaa na uzinduzi wa albamu yao ya Mubhopeghe Pa Finganilo (Kimbilieni kwenye ahadi) yenye nyimbo nane.
Kwa mujibu wa Mchungaji wa Kanisa wa EAGT, Zacharia Mwakasaka kambi hiyo inashirikisha waimbaji ambao ni Maaskofu, Wachungaji na viongozi mbalimbali wa dini waliomo kwenye Kwaya hiyo.
Mwakasaka alisema uzinduzi huo unashirikisha waimbaji, maaskofu na wachungaji waliopita kwenye mikono ya mzee Amulike Mwakiteka (84).
Mwakasaka alisema kupitia uzinduzi huo waumini mbalimbali watajionea viongozi hao ambao wanaongoza makanisa mbalimbali hapa nchini.
Mwakasaka alizitaja nyimbo zilizoko kwenye albamu hiyo ni pamoja na Mubhopeghe Pa Finganilo, Lazaro, Ilisubha ‘Jua Linachomoza’, Yesu alipokwenda, Jesu Bho Ikufyuka ‘Yesu alipopaa’, Matendo, Gwe Kyala Mwikemo ‘Mungu Mtakatifu’ na Nasobhile ‘Nilikuwa nimepotea Msituni’
Mwakalebela mgeni Rasmi Iringa
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Fredrick Mwakalebela Desemba 26 anatarajia kuwa mgeni rasmi kwenye Tamasha la Krismasi mkoani Iringa.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama Mwakalebela anatarajia pia kuwaongoza waumini mbalimbali mkoani humo kwa lengo la kumtukuza Mungu kupitia waimbaji mbalimbali hapa nchini.
Msama alisema Mwakalebela atafanikisha lengo la kusaidia wenye uhitaji maalum kama Yatima, Wajane na walemavu ambao wanahitaji msaada mkubwa kutoka kwa wadau mbalimbali.
Msama alisema Mwakalebela ni mdau ambaye anatakiwa aendane na kauli mbiu ya Tanzania ni yetu, Tuilinde na Kuipenda ambayo inachochea wadau ambao wanatakiwa kusaidia wadau hao.
Tamasha hilo linatarajia kuanza Desemba 25, kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya kabla ya kuhamia Iringa na kumalizia Desemba 28 Wilayani Songea kwenye uwanja wa Majimaji.
0 comments:
Post a Comment