OFISI ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
imetangaza kutoa vibali vya ajira 10,184 ili kuziba nafasi zilizoachwa
wazi na watumishi wa umma waliobainika kughushi vyeti vya elimu,
imefahamika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini Ofisi ya Rais, Utumishi, Florence Temba, ilieleza kuwa agizo
hilo linazihusu Mamlaka za Serikali za Mitaa, Sekretarieti za Mikoa,
Wakala wa Serikali, pamoja na Taasisi na Mashirika ya Umma.
Ilimnukuu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Angela Kairuki akitoa agizo hilo wakati akizungumza
katika kikao kazi na watumishi wa Umma wa Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar
es Salaam jana.
“Mgawanyo wa vibali vya ajira umezingatia upungufu uliojitokeza baada ya
kukamilika kwa zoezi la uhakiki, vipaumbele vya Taifa kwa sasa na
upatikanaji wa watumishi kutoka katika soko la ajira,” alisema Kairuki.
Kairuki aliongeza kuwa taratibu za kukamilisha mgawo wa nafasi za ajira
4,816 zilizosalia unaendelea ili kuwezesha wizara na taasisi nyingine
zilizokamilisha uhakiki wa watumishi wa umma hivi karibuni kuajiri
watumishi wapya kuziba nafasi wazi zilizojitokeza.
Alieleza kuwa serikali imetoa kibali kuajiri watumishi wapya 15,000 ili
kuziba pengo lililosababishwa na kuondolewa kwenye orodha ya malipo ya
mishahara kwa watumishi wa umma waliobainika kughushi vyeti baada ya
zoezi la uhakiki.
“Watumishi wa umma watakaoajiriwa kuziba nafasi hizo wanatarajiwa
kuripoti kazini kuanzia mwezi Agosti, 2017,” alieleza Waziri Kairuki, na
kuongeza kuwa utaratibu wa ajira mpya za serikali upo palepale na
amewataka wananchi kutokuwa na wasiwasi wowote wa ajira hizo.
“Napenda kusisitiza kuwa vibali tulivyovitoa leo ni vile vilivyoziba
pengo la walioghushi vyeti, naomba wananchi watambue kuwa suala la ajira
mpya bado liko pale pale kama serikali ilivyojipanga,” alisema Kairuki.
Aprili mwaka huu, Rais John Magufuli alipokea ripoti yenye orodha ya
watumishi wa umma ambao kati yao wanadaiwa kuwa na vyeti pungufu, vyenye
utata na vya kughushi kutokea kwa Waziri Kairuki.
Waliokuwa na vyeti vya kughushi walikuwa 9,932, na Rais aliapa kwamba
hawatarudi kazini. Rais Magufuli aliagiza kufutwa kazi kwa wote
waliotajwa kwenye ripoti hiyo na kuzuia mishahara yao ya mwezi huo,
lakini hata hivyo bado mlango uliwekwa wazi kwa wenye pingamizi na wapo
waliokataa rufaa huku wengine wakienda kwenye mamlaka husika kutafuta
ufumbuzi wa suala hilo.
Wiki iliyopita akiwa Dodoma, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro alitangaza kuwa
wiki hii serikali itatoa vibali 3,000 vya ajira katika sekta ya afya
vikiwemo vya madaktari na wauguzi pamoja na maofisa hesabu 535 kwa ajili
ya vituo vya afya vya kata ili washughulike na ukusanyaji wa mapato
kwenye vituo vya afya na zahanati.
Chanzo-Habarileo
0 comments:
Post a Comment