Solomon ambaye pia ni mchungaji anasema kuwa kipaji chake amepewa na Mungu japo anaweka na jitihada zake binafsi.
Nyimbo zake nyingi anajifunza kutoka kwa waimbaji wa injili Tanzania
kwani wana nafasi ya kwanza katika soko la muziki huo Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Solomon mwenye asili ya DRC akitokea Goma Mashariki mwa mji huo
akizaliwa katika familia ya kumjua Mungu japo anasema kuwa baba yake
alikuwa na wake wawili.
Anasema kuwa aliondoka nchini Congo na kuachana na wazazi wake mwaka
2003 ambapo alielekea nchini Uganda na kukaa kwa miaka mitatu na nusu
ndipo alipokutana na marehemu Angela Chibalonza aliyemuwezesha na
kumpokea Nairobi nchini Kenya.
“Angela Chibalonza ndiye aliyefungua njia katika maisha yangu ya uimbaji
japo wakati nakutana nae nilikuwa katika harakati za kurekodi albamu
yangu ya Sijaona rafiki kama Yesu, nimesalia sana katika kanisa la
Chibalonza mpaka mauti yanamkuta na siwezi kumsahau ameninyanyua,”
anasema.
Mwimbaji huyo mwenye ndoto nyingi ikiwemo ya kutaka kufungua kituo cha
watoto yatima nchini Tanzania anasema kuwa anaipenda sana nchi hii na
ndio sababu ya kutoa misaada mara kwa mara.
“Watanzania hawana mioyo ya kinafiki, ni wakarimu, wacheshi na wenye
upendo ndio sababu mimi napenda kuwa Tanzania na kutoa misada ikiwemo
kuweka kituo cha kulea watoto yatima” anasema Solomon.
Solomon Mukubwa anasema akiwa na miaka 12, alipata matatizo ya uvimbe katika mkono wake wa kushoto.
“Uvimbe huo ulikuwa wa ajabu sana na hakuna aliyefahamu chanzo kilikuwa
ni nini? Niliugua kwa muda wa miaka mitatu,”anasema solomon.
Muimbaji huyo anasema wazazi wake walihangaika kumpeleka kwa wataalam wa
hospitali mbalimbali na hata kwa waganga wa kienyeji bila mafanikio, na
anasema kuwa baada ya muda huo kupita ilianzishwa hospitali moja na
Wazungu karibu na nyumbani kwao, na ndipo wataalam wa hapo waliposhindwa
na kushauri akatwe mkono kwa lengo la kunusuru uhai wake.
Solomon anasema ugonjwa wa mkono wake ulitokana na mama yake wa kambo
kuwachukia yeye na ndugu zake ndipo mama huyo alitaka kuwaua.
“Mkono wangu ulivimba sana na baadae ukaoza hiyo ndio sababu ya kukatwa
mkono wangu, unajua shetani ni mjinga sana alinitesa kwa miaka mitatu
ndiyo sababu ya kuimba wimbo wa Mungu mwenye nguvu,” anasema.
Solomoni aliendelea kusema kuwa hakuna
mtu aliyejua kuwa uvimbe huo umetokana na nini lakini hapo baadae
ilidhihirika wazi kuwa mama yake wa kambo ndie aliyemroga na
kumsababishia tatizo hilo kwani baadae alikuja kukiri na kueleza
ukweli.
Solomoni ambaye kwa sasa maskani yake yapo jiji la Nairobi nchini Kenya
anasema wimbo wake wa Mfalme wa Amani aliutunga ili kumtukuza Mungu
baada ya kumuepusha na kifo ambacho kingempata baada ya mama yake wa
kambo kumroga na kusababisha mkono wake kuvimba na kutibiwa na madaktari
bingwa bila mafanikio na hata alipoenda kwa waganga wa kienyeji pia
hakupona.
“Wimbo wangu wa Mfalme wa amani niliamua kuuimba baada kuvuka katika
shida hizo na albamu yangu kuipa jina la Mungu mwenye nguvu, na kuna
maneno niliweka kwenye kibao hicho kwamba, ukiwa na shida usiende kwa
waganga wa dunia, mwite mfalme wa amani, yeye anajibu maombi,” anaeleza
Solomoni Mukubwa.
Baada ya kupona mkono wangu, mama
yangu wa kambo alikiri kunifanyia kitendo hicho, lakini mimi nilipookoka
nilimsamehe, baada ya muda mfupi naye aliokoka kutokana na pigo kali
alilopata kwani mwanaye aliumia jicho alipokuwa anachezea chelewa kwenye
moto ambalo uliruka na kuharibu kabisa jicho lake,”anasema.
Solomoni Mukubwa ambaye ni moja ya waimbaji maarufu wa muziki wa injili
Afrika ya Mashariki na Kati alizaliwa miaka 33 iliyopita na ameoa,
anasema kuwa anaililia nchi yake na hasa eneo analotoka ndio maana
amepanga kwenda kuhubiri ili vita iishe.
“Nawaomba viongozi wa nchi yangu wakae waone ni jinsi gani watasuluhisha
na kuwasaidia watu wangu wa Kongo hasa Goma ambako kuna
machafuko,”anasema.
Akizungumzia muziki wa injili kutumika kama biashara anaeleza kuwa
huduma ya injili ni kazi kama kazi nyingine lakini cha muhimu ni mtu
atawale fedha sio fedha zimtawale.
Anaeleza pia kuingia studio kunahitaji fedha ila fedha haziwezi kumtenga
mtu na Mungu nivema watu wakatambua kuwa muziki wa injili ni ajira
tosha kabisa na kusema kuwa kwakwe yeye akipata mahitaji ya muhimu
inatosha kabisa kumtumikia Mungu.
Solomoni ana albamu mbili ambazo ni ‘Sijaona Rafiki, ‘Mungu mwenye nguvu’ na ‘Kwa utukufu wa Mungu.’
0 comments:
Post a Comment