PADRI AFARIKI BAHARINI WAKATI AKIOGELEA
Mkuu wa Shirika la Kitawa la Consolata la Kanisa Katoliki nchini, Padri Salutaris Massawe (pichani) amefariki Dunia baada ya kuzidiwa na maji ya Bahari wakati akiogelea katika ufukwe wa Pwani ya Bagamoyo Oktoba 25.
Padre huyo ambaye alikuwa yupo Bagamoyo kwa shughuli za shirika lake, alizidiwa na maji hayo ambayo yalimchukua majira ya alasili ya siku hiyo wakati alipokuwa akiogelea pamoja na wageni wa shirika hilo walioitembelea Bagamoyo.
Mwili wa Marehemu Padri Salutaris Massawe ulipatikana jana asubuhi katika fukwe hiyo ya Bagamoyo.
Akizungumzia tukio hilo mbele ya Ripota Wetu, Katibu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Padri Joseph Masenge alikiri kutokea kwa kifo cha Padri huyo, ambapo padri huyo alifariki baada ya kuchukuliwa na maji alipokuwa akiogelea juzi saa tisa alasiri (kwa saa za Afrika Mashariki) na mwili wake kuonekana jana asubuhi ufukweni.
Padri huyo alikuwa akiogelea baharini karibu na Msalaba Mkuu wa Bagamoyo
Hadi jana mchana Padri Masenge alisema walikuwa katika maandalizi ya kuusafirisha mwili wa Padri Salutaris Massawe kuja Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuuhifadhi wakati mipango ya mazishi ikiandaliwa.
Naye, Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam,Eusebius Nzigirwa alisema kifo cha padri huyo kimeacha pengo kubwa kwani wamepoteza mtu mchapakazi na aliyefanya kazi kwa mipango.
Alisema anamfahamu Padri Massawe kwani aliwahi kufanya kazi katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam kabla ya kuchaguliwa kuwa Mkuu wa shirika hilo ambapo aliwajibika vizuri katika kusimamia majukumu yake.
Alisema kwa taarifa alizozipata awali, Padri huyo alikwenda Bagamoyo na wageni wa shirika ambao walitaka kupata historia ya jinsi Ukristo ulivyoingia nchini pamoja na historia nzima ya Ukristo.
0 comments:
Post a Comment